KOCHA wa Yanga, Mbrazil Marcio
Maximo amewaaga rasmi leo asubuhi wachezaji wa timu hiyo kwenye mazoezi
uwanja wa Sekondari ya Loyola huku akitarajia kuvuna zaidi ya Milioni 20
ndani ya klabu hiyo ikiwa ni mshahara wake wa dola 1200 na yupo kwenye
harakati za kudai fidia ya kuvunjiwa mkataba na kuletwa mrithi wake
kabla uongozi wa klabu hiyo haujamaliza nae.
Hata hivyo, tayari Maximo ameaga
wachezaji wake kwenye mazoezi ya asubuhi leo ambapo mazoezi hayo
yaligeuka shubiri baada ya Maximo kuwakusanya wachezaji wake na
kuwambia kuwa kuanzia leo sio kocha wa timu hiyo tena na kuwatakia
maisha mema ndani ya klabu hiyo ya Jangwani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
wachezaji wa klabu hiyo ambao pia hawajaridhishwa na uamuzi wa uongozi
wa klabu hiyo kumuacha mshambuliaji Hamis Kiiza na kumsajili Amis
Tambwe.
Mmoja wa wachezaji hao alisema “Ni kweli kocha ametuaga asubuhi daa! ndio hivyo tumesikitika lakini hatuna jinsi.”
Naye mchezaji mwingine ambaye
hakutaka jina lake litajwe alisema “Inaumiza sana jana (juzi) tumefanya
nae mazoezi vizuri kabisa tena amechangamka kama kawaida kumbe nyuma
kuna mambo yanaendelea, leo asubuhi tumeenda mazoezi kama kawaida
tukijua tunafanya mazoezi matokeo yake anasema acheni kila kitu kaeni
hapo nataka kuzungumza na nyinyi.
“Uwezi kuamini kidogo machozi
yanitoke pale aliposema kuanzia leo yeye sio kocha wetu tena, dah
inaumiza sana, mtu ambaye mmemzoea mnafanya nae kazi kuondoka, ndo hivyo
wakubwa wemeshaamua bwana wenye timu yao.
Wakati huyo akisema hayo, mchezaji
nguli wa timu hiyo yeye alisema “Hakuna mchezaji kwa kweli
aliyependezwa na kitendo cha uongozi, yani kwenye mazoezi asubuhi
ilikuwa kama msiba, ‘mood’ ya kufanya mazoezi iilisha kabisa, yani
hakuna aliyekuwa na hamu ya kuendelea na mazoezi.
“Tumefanya kidogo mazoezi
tukaondoka, ukiangalia ni sawa tumefungwa cha muhimu ilikuwa ni kukaa
chini na kuzungumza na kuangalia cha kufanya, kama kuna mapungufu basi
yafanyiwe kazi, mimi sijaona haja ya kumfukuza kocha hasa kipindi kama
hichi.”
Meneja wa timu hiyo Hafidhi Saleh
alikiri Maximo kuaga wachezaji kabla ya mazoezi ya timu hiyo kuanza
akiwapa moyo wajitume kwa kuwa ni wachezaji wazuri na timu ni nzuri na
kuwataka kuongeza bidii ili wafike mbali.
“Kwa kweli inasikitisha hakuna
mchezaji wala mtu aliyefurahia, kama yupo labda kimoyomoyo ila dah
imetuumiza, ni mazoea cha muhimu tugange yajayo hayo mengine tuwaachie
viongozi.”alisema Saleh
Saleh alisema kuwa tayari kocha
Hans van Der Pluijm ambaye amefikia kwenye hoteli ya Tansoma jana
alikuwa kwenye mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo ili aichukue nafasi
ya mbrazil Marcio Maximo ambaye amekumbwa na kipunga cha kutimuliwa
baada ya kunyukwa mabao 2-0 katika mechi ya mtani Jembe, akiwa ni kocha
wa pili kutimuliwa Yanga baada ya matokeo ya mtani jembe mwaka jana
alitimuliwa Ernie Brandts baada ya kunyukwa mabao 3-1 na nafasi yake
kuchukuliwa na Pluijim ambaye nae hakukaa sana akaikacha timu hiyo baada
ya kupata kibara nchini Saudi Arabia.
Wakati huo huo, uongozi wa Yanga
umegwaya mchezaji Andry Countinouh kuvunja mkataba wake baada ya kuwa
wangelazimika kuvunja kibubu cha Sh185 milioni ili kumlipa fidia ya
mshahara wake ambao ni dola 2800 kwa mwezi.
Katika hatua nyingine, pamoja na
Yanga kumfungashia virago Emerson De Oliveira Neves Roque imemuombea
kibali cha usajili wa kimataifa (ITC) kutoka Bonsucesso Brasil kwenda
Yanga.
Mkurugenzi wa mashindano ya TFF, Boniface Wambura alisema kuwa TFF haina taarifa za Yanga kumuacha mbrazili huyo.
No comments:
Post a Comment