Friday, July 25, 2014

Siri utupaji viungo vya maiti yabainika Kumbe vilitoka Hosipitali hii??

Makamu Mkuu wa Chuo cha International Medical and Technological University (IMTU), Profesa PV Prabhak Rao (mwenye koti la blue)  na viongozi wengine wakisindikizwa na polisi kuingia kwenye Kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam jana, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na upatikanaji wa viungo vya binadamu eneo la Mpigi Bunju. Picha na Rafael Lubava 

Dar es Salaam. Wakati ikibainika kuwa viungo vya miili ya binadamu vilivyookotwa juzi katika Bonde la Mto Mpiji nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam vilitoka katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), jana Jeshi la Polisi liliwatia nguvuni watumishi wanane wa chuo hicho kuhusiana na sakata hilo.
Kukamatwa kwa watumishi hao kumeelezwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa ni baada ya uchunguzi wa awali kubaini kuwa viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa katika maabara ya IMTU.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni eneo la Bonde la Mbweni Mpiji ambako iligundulika mifuko ya plastiki 85 yenye mabaki ya viungo vya binadamu.
Kutokana na tukio hilo, Polisi imeunda jopo la wapelelezi saba likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Jafari Mohamed kusaidiana na daktari wa jeshi hilo kufanya uchunguzi wa miili hiyo.
“Katika uchunguzi wetu tulibaini kuwa hivyo viungo vya binadamu vilitolewa katika Chuo cha IMTU na kusindikizwa na mfanyakazi wa ngazi ya juu kwa ajili ya  kutupwa eneo la Bonde la Mbweni Mpiji,” alisema Kova.
Alisema mifuko hiyo ilikuwa myeusi ikiwa na viungo vya aina mbalimbali vikiwamo vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali.
“Viungo hivyo havikuwa na harufu wala uvundo wa aina yoyote na vilionekana vimekaushwa na kukakamaa,” alisema.
Alisema katika eneo hilo walikuta vifaa vinavyotumika hospitali kama glovu, nguo maalumu (apron) 20 na karatasi mbili zenye maswali ya kujibu.
Kova alisema viungo hivyo vilichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema jeshi hilo limefungua jalada la uchunguzi ili kujua sheria gani imevunjwa na kwa nini viungo hivyo vilitupwa hapo na kwa nini wasitumie utaratibu mzuri wa kuhifadhi na kwamba endapo kuna makosa ya kisheria, hatua zitachukuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Muhimbili wapokea mabaki
Meneja Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema jana kuwa hospitali hiyo imepokea vifurushi 40 vyenye mabaki ya miili ya binadamu na kuhifadhiwa wakisubiri maelekezo ya polisi... “Hili ni suala la polisi, ninachoweza kusema ni kweli tumepokea vifurushi hivyo jana (juzi) usiku.”Chanzo MWANANCHI

No comments:

Post a Comment