Friday, June 6, 2014

BINTI ALIYEFARIKI NA KUZIKWA ATINGA KWAO ARUSHA AKIWA HAI. SOMA KISA KIZIMA HAPA


Stori: Joseph Ngilisho, ARUMERU/GPL

HOFU ya ushirikina imetikisa Mkoa wa Arusha kufuatia tukio la hivi karibuni ambapo mwanafunzi wa Chuo cha Kompyuta jiji hapa, Witness Obed (21) aliyefariki dunia Aprili 12, mwaka huu na kuzikwa kwenye makaburi ya nyumbani kwao Kijiji cha Nanja, Kata ya Moshono wilayani Arumeru, Arusha kuibuka akiwa hai.


Witness Obed (21) aliyefariki dunia Aprili 12 mwaka huu na kuzikwa kwenye makaburi ya nyumbani kwao Kijiji cha Nanja, mkoani Arusha na kuibuka akiwa hai tena.

Binti huyo aliibuka kwao hivi karibuni akiwa mpole na kuwafanya baadhi ya watu, wakiwemo wazazi wake kutimua mbio kwa hofu.
Watu kutoka maeneo mbalimbali jijini hapa  wamekuwa wakimiminika nyumbani kwa wazazi wa binti huyo kwa lengo la kumshuhudia kwa vile ndugu walishaamini kuwa, mpendwa wao huyo alishakufa na alizikwa.


Umati wa watu ukiwa katika hali ya mshangao kutokana na tukio hilo.


UWAZI LATIA TIMU NYUMBANI

Baada ya kusikia taarifa hizo, Uwazi lilifunga safari mpaka eneo la tukio na kumshuhudia binti huyo kisha likaenda kwenye kaburi alilozikwa.


Kwenye kaburi hilo, msalaba wenye kuonesha siku yake ya kuzaliwa (1992) na kufa (12, Aprili, 2014) ulikuwa bado umesimama imara huku kaburi lenyewe likionesha dalili ya kutitia kidogo.

BABA MZAZI ASIMULIA

Akisimulia mkasa huo kwa mshangao mkubwa, baba mzazi wa binti huyo, Obed Leiyo alisema:

“Ilikuwa Aprili mwanzoni, binti yangu alitoweka nyumbani  baada ya kurudi kutoka chuoni majira ya saa 2 usiku akiwa amechelewa.


Hili ni kaburi alipozikwa Witness Obeid Leiyo.

Mimi kama mzazi nilimfokea kwa kuchelewa kwake kurudi nyumbani.

“Yeye kwa hasira zake alizunguka nyumba akaondoka muda huohuo na hakurudi kabisa hapa nyumbani.


“Siku iliyofuata tulianza kumtafuta maeneo mbalimbali bila mafanikio, tukatoa matangazo kwenye vyombo vya habari lakini binti yangu hakuonekana.”

TAARIFA ZAFIKA, KAFA

Mzazi huyo aliendelea kusema: “Siku moja tulipata taarifa kwamba kuna mwili wa msichana umeonekana  katika Kijiji cha Bwawani hapahapa Arumeru.

“Mimi pamoja na ndugu wengine tuliamua kwenda katika kile kijiji. Tulipofika tuliambiwa ni kweli mwili wa msichana uliokotwa lakini wananchi wakauzika.”
WAFUKUA KABURI

Baba huyo anaendelea: “Niliamua kwenda Kituo cha Polisi cha Usa River ambako niliomba kibali kwa ajili ya kufukua kaburi na kuutoa mwili ili kuutambua kama ni binti yangu au la!
“Nilipewa kibali, tukafukua kaburi na kutoa mwili. Nilimtambua kuwa ni binti yangu kutokana na alama mbalimbali alizokuwa nazo, ikiwemo rangi kwenye kucha na sehemu ya kushoto ya uso ilikuwa nyeusi kwa sababu aliwahi kupooza.

Witness akiwa na baba yake mzazi, Bw. Obeid Leiyo Mara baada ya kurudi nyumbani akiwa hai.

MWILI WASAFIRISHWA, WAZIKWA

Baba huyo wa Witness alizidi kueleza kuwa waliusafirisha mwili huo hadi nyumbani kwake Moshono na kuandaa taratibu za mazishi ambapo Aprili 23, mwaka huu mwili ulizikwa.
AIBUKA GHAFLA

Hata hivyo, Obed anasema alishangaa siku ya tukio kumwona binti yake huyo akiibuka nyumbani hapo akiwa hai jambo ambalo lilimshangaza na kumfanya akimbie kwanza na baadaye kufanya mawasiliano naye.
BINTI ASIMULIA

Akizungumza na Uwazi, binti huyo alikiri kutoweka nyumbani kwao Aprili 15, mwaka huu na kwenda kusikojulikana.
Alisema hakujua kilichoendelea baada ya kuondoka nyumbani lakini baadaye alibaini kuwa alikuwa katika Kijiji cha Olkokola wilayani Arumeru na alikwenda kwenye nyumba ya mwanamke mmoja asiyefahamiana naye akamuomba maji ya kunywa.

“Nilifika kwenye nyumba moja nikamkuta mama mmoja, nikamwomba maji ya kunywa akaenda kuniletea. Nilikunywa huku amenisimamia, lakini maji yalikuwa machungu sana, nikamrudishia, akanilazimisha ninywe kwa kunisukumia kikombe kinywani. Nilipomaliza nilipoteza fahamu.

“Baadaye nilizinduka, nikaendelea kuishi palepale nyumbani kwa yule mama  lakini sifahamu nilikuwa nafanya nini.

“Juzi ndiyo nikashangaa 

kujikuta nimerudi nyumbani, mimi sijui nini kilikuwa kikiendelea,” alisema binti huyo.
MAJIRANI NAO

Majirani kadhaa waliokuwepo nyumbani kwa Obed walilielezea tukio hilo kwamba ni la ushirikina huku wakisema ni jambo la kuogofya ambalo halikuwahi kutokea kijijini hapo kabla.
Wengine walisema kuwa binti huyo alifufuka na wengine walisema alichukuliwa msukule.

“Hili si suala la kawaida lazima kuna ushirikina kwani huyu binti tulishamzika na wazazi wake walimtambua kabisa kuwa ni yeye baada ya
kuambiwa alikutwa amekufa, sasa hebu fikiria tangu tumezika mbona hakuna mtu aliyekuja na kusema na yeye alipotelewa na binti yake halafu cha ajabu hilo kaburi mbona limebonyea? Atakuwa amefufuka,’ alisema mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Amina Liwa.

Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Usa River, Benedict Mpujila amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unafanyika.

KUMBUKUMBU

Mapema mwaka jana tukio la kishirikina liliibuka katika wilayani Arumeru eneo la Kwa Mrefu ambapo mtu mmoja alidaiwa kudondoka na ungo, muda mfupi baadaye alitoweka na kwenye ungo kubaki mayai na kuku mweupe.

No comments:

Post a Comment