Bunduki
ya kivita aina ya Sub Machine Gun (SMG) iliyotumika kumuua
mfanyabiashara tajiri wa Mirerani, Erasto Msuya, ilinunuliwa kwa Sh4
milioni nchini Kenya, Mahakama imeelezwa.
Imeelezwa
pia kwamba wauaji wanne waliokwenda eneo la tukio kutekeleza mauaji
hayo, walilipwa Sh5 milioni kila mmoja na washirika wao wakilipwa Sh3
milioni kila mmoja.
Hayo yamo
katika maelezo ya mashahidi 57 kwa washtakiwa yalisomwa mbele ya Hakimu
Mkazi wa Mkoa Kilimanjaro, Munga Sabuni juzi na mawakili wa Serikali,
Stella Majaliwa na Florentina Sumari waliokuwa wakipokezana kuanzia saa
4:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni.
Msuya
aliyekuwa anamiliki vitega uchumi kadhaa, aliuawa kwa kumiminiwa risasi
Agosti 7, mwaka jana saa 6:30 mchana Mijohoroni wilayani Hai,
Kilimanjaro na katika maelezo yake, mtaalamu aliyeufanyia uchunguzi
mwili wa marehemu, Dk Paulo Christopher alisema ulikuwa na matundu 26 ya
risasi yaliyotokana na risasi 13 zilizoingia na kutokea upande wa pili
zikichanachana utumbo, mapafu, ubongo na bandama.
Ushahidi huo unadai kuwa katika eneo la tukio, polisi waliokota maganda 22 ya risasi za SMG.
Mtaalamu
wa makosa ya kijinai ya kompyuta, Koplo William Obeid alieleza kuwa
katika kufanikisha mauaji hayo, laini mpya tano za Airtel zilisajiliwa
kienyeji, zote zikiwa na jina la Motiti Ndoole na laini iliyotumika
kumvuta marehemu eneo la tukio ilikuwa 0682405323.
Katika
ushahidi huo, Inspekta Samwel Maimu alidai kuwa washtakiwa walikiri kosa
na kueleza kuwa bunduki aina ya SMG ilinunuliwa Namanga, upande wa
Kenya. Inspekta Maimu alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza, Shariff Mohamed
ndiye aliyetoa Sh4 milioni za kununua silaha hiyo na kutoa fedha za
kusajili line mpya tano za simu.
Pia
alidai kuwa mshtakiwa huyo, ndiye aliyetoa Sh3,350,000 zilizotumika
kununulia pikipiki mbili moja aina ya Toyo na nyingine King Lion
zilizotumiwa na wauaji siku ya tukio.
Katika
maelezo hayo yaliyosomwa mahakamani, mshtakiwa wa kwanza (Shariff),
anadaiwa kueleza namna alivyotoa maagizo ya kusajiliwa kwa line mpya.
Mshtakiwa
huyo anadaiwa kueleza kuwa mshtakiwa wa saba, Ally Mussa ndiye
aliyemshauri atoe jiwe moja la Tanzanite litakalotumika kumshawishi
marehemu Msuya. Katika maelezo hayo, ilidaiwa kuwa ndiye aliyelipa Sh4
milioni za kununua bunduki hiyo ya SMG na kwamba siku ya tukio aliibeba
kwa gari lake hadi eneo la tukio na kuwakabidhi wauaji.
baadhi ya watuhumiwa wa mauaji hayo |
Katika
ushahidi huo, mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa anadaiwa kueleza kuwa
yeye ndiye aliyemmiminia risasi marehemu ambazo hajui idadi yake na
kwamba bunduki hiyo aina ya SMG waliinunua Namanga na ilihifadhiwa
nyumbani kwa Shariff sambamba na pikipiki zilizotumika.
Katika
maelezo yake, mshtakiwa wa saba, Ally Mussa au Majeshi anadaiwa kueleza
kuwa ndiye aliyepewa kipande cha madini na kwenda kumuuzia marehemu
hotelini kwake SG Resort siku moja kabla ya mauaji.
Chanzo cha habari hii ni Libeneke la Kaskazini
No comments:
Post a Comment