Thursday, January 9, 2014

HUU NDIO MPANGO MZIMA WA KUTESWA KWA MWENYEKITI WA CHADEMA

MWENYEKITI wa Chadema wilayani Temeke, jijini Dar Joseph Yona,33, ameeleza A-Z sakata la kutekwa, kuteswa kwake na vijana sita wakati akienda nyumbani kwake Mtoni kwa Azizi Ally.
Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Temeke na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Joseph Yona akipelekwa Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) kutoka wodini.
Akisimulia mkasa huo kwa mwandishi wa gazeti hili juzi Jumanne akiwa Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Yona ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu, Taifa Chadema alikuwa na haya ya kusema: “ Majira ya usiku nikiwa na baadhi ya vijana wa Chadema Tawi la Ukombozi lililopo karibu na kwangu maeneo ya Benki Klabu, Mtoni kwa Azizi Ally tulikuwa tukiongea. 

“Ilipofika saa sita tukatawanjika mimi nikawa naelekea nyumbani, kabla sijafika mbali nikashitukia vijana sita wakinivamia na kunikaba kisha kunivua tisheti na kunifunga usoni,  wakaniingiza katika gari ambalo walikuwa wamepaki pembeni.
“Nilipowauliza mnanipeleka wapi? Wakawa wanajifanya ni askari kwani walikuwa wanasema, ‘tumeshamkamata, tunamleta huko kituoni afande’, tukiwa njiani waliniambia niseme Zitto ni msaliti badala yake nikawaambia kuwa hilo waulizeni viongozi wa juu. 

“Baada ya kuona tumesafiri kwa muda mrefu niliwauliza mbona hatufiki kituoni? Wakasema wewe ndiye tulikuwa tunakutafuta, utakiona cha moto, usipokufa utawasimulia wenzako. Walinipeleka mpaka kwenye msitu, baadaye ikafahamika kuwa ni Ununio, Tegeta wilayani Kinondoni. Huko walinipiga sana kisha kunitelekeza katika pori hilo nikiwa nimezimia. 

“Baadaye  nilipata fahamu nikajikokota kwa taabu hadi kwenye nyumba moja, nikagonga lakini hawakunifungulia. Nikaenda nyumba ya pili kugonga napo hawakunifungulia. Nyumba ya tatu nilipoigonga wakanifungulia. Walinishangaa na kuniuliza kulikoni umelowa damu? Nikawaeleza kilichonipata. 

“Watu hao waliwasiliana na polisi ambao walikuja na kunichukua mpaka hapa Muhimbili nilipofanyiwa uchunguzi nikahamishiwa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi). Lakini kule porini wale watekaji walichukua vitu vyangu kama vile simu mbili na pochi yenye fedha na waliondoka nazo.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, SACP Engelbert Kiondo akiongea na mwandishi wetu ofisini kwake alikiri kutokea kwa tukio hilo. “Msako mkali unaendelea ili kuwabaini na kuwakamata wale waliohusika na unyama huo ili wafikishwe mahakamani,” alisema Kiondo.

No comments:

Post a Comment