Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro,Robert Boaz
Wakati kundi la wafanyabiashara wakubwa wa madini jijini Arusha wakiwa wamekusanyika nyumbani kwa mwenzao, Erasto Msuya, aliyeuawa kikatili juzi eneo la Mjohoroni, wilayani Hai, taarifa za kiuchunguzi zinasema kuwa kuna kila dalili kuwa mauaji hayo ni matokeo ya kuzidiana kete katika biashara zisizo rasmi.
Jana NIPASHE ilifika nyumbani kwa marehemu eneo la Sakina jijini humo na kukuta kundi kubwa la wafanyabiashara likiwa linakutana kujadili shughuli za mazishi wakati mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika hospitali ya Seliani jijini hapa.
Jiji la Arusha na viunga vyake kumekuwa na uvumi na taarifa ambazo hazikanushiki kuwa katika biashara ya madini ya Tanzanite usiri na kudhulumiana vimekuwa ni sehemu ya shughuli hiyo kiasi cha kusababisha visasi na hata mauaji.
“Wewe fikiria inakuwaje mtu abebe Sh. milioni 100 peke yake aende porini kote kule kufanya biashara. Yaani anakwenda kununua madini porini, hana ulinzi, hana risiti hana nini… hapa aliitwa kuwa kuna mzigo kumbe wamemlengesha,” alisema mkazi mmoja wa Arusha ambaye aliomba kusitiriwa jina lake.
Aliongeza kuwa: “Unajua hawa wafanyabiashara bwana wana mambo yao mengi. Kwa sasa ni vigumu kusema hasa nini kimemtokea, lakini najua kwa miaka mingi mambo yao mengi ni deal (magendo) tu. Hata hapa unaona wazi kuwa maswali ni mengi kuliko majibu.”
Naye mkazi wa Kaloleni Arusha anayejishughulisha na biashara ya utalii alisema kuwa ukiwaita wafanyabiashara wa madini wote hasa wenye vitega uchumi vikubwa jijini hapa na kuwauliza nyaraka za shughuli za madini utashangaa kwa kuwa kila kitu kinafanyika kama watu wanaohama kesho.
“Si unajua bwana hata Benki Kuu ilikwisha kutoa maagizo kuwa hakuna malipo yanaozidi Sh. milioni 10 yanalipwa kwa cash (taslimu)? Sasa kama marehemu alikuwa na Sh. milioni 100 kama inavyoelezwa ina maana alikuwa anavunja sheria na pia anajihatarishia usalama wake mwenyewe,” alisema mkazi huyo huku akiomba jina lake lisitajwe kwa kuwa biashara za Arusha zina siasa zake.
Kijana mmoja mkazi wa Usa River, Uria Nnko, ambaye amekuwa kwenye shughuli ya madini kwa kitambo sasa, alisema kuwa kwa muda mrefu sasa biashara ya Tanzanite jijini Arusha inategemea sana vijana aliosema “wanapiga mzigo” kutoka mgodi wa Tanzania One.
Nnko alisema kuwa kwa hali inavyoonyeshwa marehemu aliitwa kwenda kununua mzigo wa namna hiyo na kwa kuwa anajua hizo shughuli zipo aliingia kichwa kichwa kumbe safari hii alikuwa amewekewa mtego na waliomuua na kumpora.
Matukio ya mauaji ya wafanyabiashara wa Tanzanite jijini Arusha ni mengi, na mara kadhaa yamekuwa yakielezwa kuwa yanafanywa kutokana na kudhulumiana au kuzidiana kete.
Biashara hiyo imeelezwa kufanywa kwa mfumo wa uuzaji dawa za kulevya kama ambazo hufanywa duniani na makundi hatari ya uhalifu kama Mafioso (mafia) ambayo kila kitu humalizwa papo kwa papo bila nyaraka za kiserikali wala kibenki.
Mbali na hisia hizo za biashara za madini kujawa na usiri mkubwa, wananchi katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wametoa maoni tofauti wengi wakimwelezea Msuya kama mtu mwema, mchapakazi na mwenye juhudi.
MATAJIRI ARUSHA
Wafanyabiashara wa madini jijini Arusha wamevitaka vyombo vya dola kuchunguza haraka chanzo cha mauaji ya kinyama ya mwenzao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wahusika.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite na Diwani wa Kata ya Mererani, Justin Nyari, alisema wamesikitishwa na kitendo cha mwenzao kukatishiwa uhai.
Alisema wanatambua mtu akizaliwa lazima afe, lakini si kama alivyofariki mwenzao.
"Tunaomba vyombo vya dola vidhibiti hili na watafute ukweli," alisema Nyari.
Alisema tayari wapo katika vikao na wanandungu na bado hawajajua mazishi ni lini, ila mwili umehifadhiwa hospitali ya Selian Medical Lutheran Center, mjini hapa.
Mfanyabiashara huyo alikuwa anamiliki mgodi wa Kalo uliopo Mererani na pia anamiliki migodi mingine miwili ya baba yake Kikaango Msuya iliopo block B Mererani.
Mbali na migodi hiyo, Erasto anamiliki vitegauchumi lukuki ikiwamo hoteli moja kubwa inayojulikana kwa jina la SG Resolt, iliyopo Sakina, jijini Arusha.
Mkoani Kilimanjaro, Polisi wamesema kwamba wamefanya uchunguzi wa kitabibu kwa mwili wa marehemu na imebainika kwamba alipigwa risasi tano.
Akithibitisha uchunguzi huo, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema licha ya uchunguzi kufanyika, lakini hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.
“Tumefanya uchunguzi na mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Upareni kama watakavyoamua, hatujamkamata mpaka sasa mtu yeyote anayehisiwa kutenda unyama huo, tunahaha kuwasaka katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara,” alisema.
Aidha, Kamanda Boaz aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuwatia mbaroni wauaji na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Eneo la Mjohoroni wilaya ya Hai alikouawa Msuya kikatili juzi karibu ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).
Tukio hilo lilitokea mchana wakati akiwa njiani kutokea Arusha kwenda Moshi kwa gari lake aina ya Range Rover lenye namba za usajili T 800 CKF.
Taarifa kutoka eneo la tukio zilidai kuwa Msuya alipigwa risasi na watu wawili wanaodaiwa kwamba walimpigia simu na kuahidiana nao wakutane eneo hilo kwa ajili ya kumuuzia madini.
Kumekuwa na habari mkanganyiko, baadhi zikisema kuwa wauaji hawakuchukua kitu chochote kuanzia gari, fedha Sh. milioni 100 zilizokuwa ndani, simu za mkononi pamoja na ipad, ilhali nyingine zikidai kuwa waliondoka na mfuko wenye fedha.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment