KATIBU wa Jumuiya ya Kiislamu nchini , Shekhe Ponda Issa Ponda,jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuumizwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni risasi kwenye bega lake la kulia wakati akiekelea katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja wa Mjini Morogoro baada ya kumalizika kwa kongamano ya Dini ya Kiislamu.
Mkasa huo ulitokea jana Jumamosi Augosti 10, mwaka huu majira ya saa 12: 15 za jioni eneo la barabara ya Tumbaku karibu na Fire, mara baada ya kumalizika kwa Kongamano la Kiislamu lililofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege, Kata ya Saba Saba , Manispaa ya Morogoro.
Shekhe Ponda alishiriki katika Kongamano hilo lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri wa Dini ya Kiislamu Mkoani Morogoro na kufanyika siku ya Idd Pili kuanza saa nane mchana hadi kumi na mbili jioni ya siku hiyo.
Kongamano hilo lilipata baraka zote kutoka Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, ambalo lilitoa masharti kadhaa ya kuzingatiwa na wazungumzaji ikiwa ni kutokashifu dini nyingine wala viongozi wa serikali.
Sakata la kutaka kutiwa mbaroni kwa Shekhe Ponda lilikuja baada ya yeye kudaiwa kukiuka masharti ya Mahakama aliyopewa wakati alipohukumiwa kifungo cha mwaka mmoja nje na kutakiwa asitende kosa lolote la jinai anapotumikia adhabu hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadalizi ya Kongamano hilo, Ustaadhi Idd Msema, alisema kuwa, Shekhe Ponda baada ya kutoka ndani ya Gari eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege alikofikia mita chache katika barabara ya Tumbaku aliteremka na wakati akitaka kuingia kwenye Gari, ilifyatuliwa risasi iliyompiga begani.
Ustaadh Msema aliendelea kusema kuwa, baada ya kupigwa risasi begani waumini waliokuwa wameambatana naye walimchukua na kumpakiza kwenye Piki Piki hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ili kupatiwa matibabu.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti huyo, baada ya kufika hospitali, waliona
anacheleweshwa kupatiwa matibabu na ndipo walipoamua kumwondoa na
kumpeleka kwenye Hospitali binafsi ambayo hakupenda kuitaja jina kwasababu za kiusalama.
Akizungumzia kwa kina hali ya Shekhe Ponda baada ya kujeruhiwa, alisema kuwa yupo hai licha ya kuumia vibaya begani na kwamba wanatarajia kumpekela katika hosipitali nyingine hususani Jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Alisema uongozi wa Umoja huo hauwezi kuweka wazi sehemu anakotibiwa kwa kuwa jambo hilo ni la kiusalama zaidi hasa wakati huu ambapo kumekuwa na hali ya sinto fahamu.
Baadhi ya walinzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro waliozungumzia tukio hilo , walikiri kuwa Shekhe Ponda aliletwa hapo kwa usafiri wa Piki piki zikiambatana na nyingine zaidi ya 50 na kuishia getini.
Walisema walimwingiza hadi mapokezi na kwamba walipoona umati mkubwa upo getini waliamua kutoa taarifa Polisi kuwa wamevamiwa na watu ambao waliwatia wasiwasi, ambapo muda si mrefu Polisi kikosi cha FFU waliwasili na gari lao Hospitalini hapo.
Hata hivyo walinzi hao walisema, baada ya kuona Askari wamefika Hospitalini hapo, baadhi ya wafuasi wa Shekhe Ponda waliamua kumnyanyua na kumbeba mabegani na kutoka naye mlango mwingine wakimlazimisha mlinzi kuwafungulia mlango na baadaye wakatokomea naye kwa usafiri wa Pikipiki kusikojulikana.
Kufikishwa kwa Sheshe Ponda katika Hosipitali ya Rufaa kulithibishiwa pia na Mwenyekiti huyo ambaye alidai kuwa waliamua kumwondoa baada ya kuchekewa kupatiwa huduma.
Baada ya tukio hilo, uvumi ulisambaa meneo mbalimbali nchini ukidai kuwa Shekhe Ponda amepigwa risasi na Polisi na kufariki dunia.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Feustine Shilongine akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi majira ya saa tatu usiku wa Augosti 10, baada ya kutokea kwa tukio hilo, alisema kuwa hapakuwa na taarifa juu ya kutokea kifo cha Shekhe Ponda.
“ Nimepigiwa simu zaidi ya 50 , zikiulizia jambo hili...kuwa Ponda amefariki dunia ...Binafasi nami ninazisikia , ujumbe umesambazwa kwenye simu za watu mbalimbali...tumezunguka kila mahali hakuna kifo wala maiti yake ...na vijana wangu wanaendelea kulifuatilia suala hili” alisema Kamanda huyo.
Juhudi za kufuatilia sakata la uvumi kifo cha Shekhe Ponda uliendelea kufanyiwa kazi na Ripota wetu huyu na usiku wa saa tano Mwenyekiti wa Kamati huyo aliweka wazi kwa kusema kuwa Shekhe Ponda yu hai isipokuwa ameumia vibaya sehemu ya bega .
“ Nipo katika eneo ambalo Shekhe Ponda anapatiwa matibabu...sehemu ambayo hatuwezi kupataja kiusalama , isipo kuwa ameumia vibaya kwenye bega lake.
"Lakini yu hai wala hajafa” alisema Msema.
Askari wa FFU wakijisogeza kati kati ya uwanja mara baada ya muda wa kongamano kumalizika.
Kutambulishwa jukwaani Shekh Ponda.
Kikosi cha FFU uwanjani
Shekh Ponda akisalimiana na Mhadhiri wa Mihadhara nchini, Ustaadhi Abubakari
Shekh Ponda akisisistiza jambo mbele ya waumini wa Dini ya Kiislamu kwenye Kongamano , Augosti 10, mwaka huu mjini Morogoro
Shekhe Ponda akiwa meza kuu kwenye kongamano hilo
Shekhe Ponda akiwa amezingirwa na waumini
Waumini wa Dini ya Kiislamu wa mjini Morogoro wakimsikiliza Shekh Ponda |
Waumini wa Kiislamu wakitawanyika uwanjani baada ya muda wa kongamano kufikia tamati.
No comments:
Post a Comment