Friday, June 14, 2013

ASKARI 15 WADAI WAMEFUKUZWA KAZI BAADA YA KUYAKAMATA MAGARI YA RAIS MSTAAFU PAMOJA NA VIGOGO WENGINE WA SERIKALINI

ASKARI 15 wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam waliofukuzwa kazi hivi karibuni kwa kosa la kupokea rushwa ili kupitisha mizigo bandarini kwa njia za magendo wameibuka na kutoa siri ya kufukuzwa kwao.


Mmoja wa askari hao akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema sababu ya kufukuzwa kwao imetokana na wao kukamata magari ya vigogo serikalini, akiwemo aliyekuwa Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ambaye anadaiwa kuwa kinara wa kukwepa kodi.

Akizungumza na gazeti hili, askari huyo alisema baadhi ya viongozi wa juu wa jeshi hilo wamekuwa wakiwasaidia wafanyabiashara wakubwa kukwepa kodi na pindi askari wadogo wanapoyakamata magari hayo hufukuzwa kama ilivyotokea kwao.

Kwa mujibu wa habari hizo, katika kesi ya kijeshi iliyotolewa hukumu ya kuwaondoa kazini askari hao, waliomba waoneshwe dereva na gari linalodaiwa kuwa lilitoa rushwa kwao kama kielelezo muhimu katika kesi yao, lakini hadi sasa gari na dereva huyo hawajapatikana.


Mashtaka ya askari hao, yalitarajiwa kusomwa na askari mmoja wa juu, lakini alipobaini kwamba hakuna ushahidi, aliamua kujiondoa na kuchukuliwa na askari mwingine ambaye ndiye aliyewasomea mashitaka.
 
“Baada ya kesi kusomwa Juni sita mwaka huu, ikatolewa hukumu ya kutuondoa kazini pasipo walalamikaji na vidhibiti kuwasilishwa katika mahakama ya kijeshi. Kwa kifupi hatukutendewa haki na tunakusudia kukata rufaa,” alisema askari huyo kwa niaba ya wenzake.

“Ukweli ni kwamba wanaofanya baiashara ya kuingiza bidhaa bila kulipia kodi ni viongozi wakubwa wa nchi hii hasa huyu kiongozi mstaafu wa Zanzibar na mkewe, sisi leo hatupo kazini na wao wanaendelea kupitisha bidhaa bandarini kwa rushwa,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, akizungumzia hatua ya askari hao kufukuzwa kazi alisema alichofanya ni kuthibitisha adhabu yao baada ya kupitishwa katika kitengo cha nidhamu ya jeshi.

“Kwangu si muhimu kujadili adhabu iliyotolewa na mahakama ya kijeshi, nilichofanya ni kuthibitisha tu na kama wanaona wameonewa, tumewaambia wakate rufaa,” alisema Wambura.

Akizungumzia madai ya kuwalinda baadhi ya viongozi katika tuhuma za kusafirisha mizigo pasipo kulipia ushuru, Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo aziwasilishe kwake.
 
Kuhusu kukosekana ushahidi pamoja na wahusika waliotumika kutoa rushwa, CP Kova, alisema hawezi kuwataja kwa kuwa walitumwa kuweka mtego wa kuwanasa askari wanaosaidia watu kukwepa kodi.

Taarifa za kukamatwa kwa askari hao, zilifichuliwa na gazeti hili na kuripoti kuwapo kwa mtandao mpana wa askari wa jeshi hilo wanaojihusisha kuwasaidia wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi.

No comments:

Post a Comment