Friday, June 14, 2013

MRISHO NGASSA KUZUIWA KUCHEZA JUMAPILI DHIDI YA IVORY COAST

KIKOSI cha Taifa Stars kitashuka dimbani keshokutwa Jumapili kuivaa Ivory Coast katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2014, lakini habari ni kuwa kiungo mshambuliaji wa Stars, Mrisho Ngassa hataruhusiwa kucheza kwa kuwa ana kadi mbili za njano.
Taarifa ambazo Championi Ijumaa imezipata kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zimesema kuwa wamepokea ujumbe kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuwa Ngassa ana kadi mbili za njano.
Taarifa hiyo imesema kuwa, kiungo huyo alipata kadi mbili za njano katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini wakati Stars ikiumana na Morocco, ambapo mchezo wa kwanza uliopigwa Machi, Stars ilishinda mabao 3-1 kabla ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 ugenini.
“Tumepokea ujumbe kutoka Caf juu ya Ngassa, ni taarifa mbaya hasa katika siku hizi mbili kwa sababu tunajua kocha alikuwa anajua atakuwa naye katika mchezo wa keshokutwa,” alisema kiongozi huyo wa TFF.
Aidha, straika wa Stars, Mbwana Samatta: “Ile ni timu tu (Ivory Coast) kama timu nyingine, sijaona sababu za kuiogopa au kuihofia, tuna asilimia kibao za kushinda ukizingatia tunacheza nyumbani, ” alisema Samatta.

No comments:

Post a Comment