Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen akiwaonesha waandishi wa habari timu
wanazocheza wachezaji wa Morocco katika vialabu vya Ulaya. (Picha na
Habari Mseto blog)
Kocha Mkuu
wa Taifa Stars, Kim Poulsen akifafanua jambo wakati akitangaza kikosi
cha wachezaji 23 watakaoingia kambini kwa ajili ya mechi ya mchujo
kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia zitakaofanyika
mwakani nchini Brazil.
Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja wachezaji 23 watakaoingia
kambini Jumamosi (Machi 16 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
mechi ya mashindano dhidi ya Morocco.
Mechi hiyo ya
mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia
zitakazofanyika mwakani nchini Brazil itachezwa Machi 24 mwaka huu
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa
Kocha Kim, wachezaji wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager wanatakiwa kuripoti kambini katika hoteli ya Tansoma,
Machi 17 mwaka huu.
Wachezaji
walioitwa ni makipa Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa
Stars, Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Mwadini
Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Issa
Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga),
Nassoro Masoud Cholo (Simba) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni
Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis
Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani
Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji
ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Thomas
Ulimwengu wa TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Mbali ya Kim,
benchi la ufundi la Taifa Stars linaundwa na Sylvester Marsh (Kocha
Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja), Dk.
Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Mtaalamu wa
tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
SEMINA ELEKEZI COPA COCA-COLA KUFANYIKA MACHI 19
Semina elekezi
kwa ajili ya michuano ya Copa Coca-Cola 2013 itafanyika Machi 19 mwaka
huu jijini Dar es Salaam. Washiriki wa semina hiyo wanatakiwa kuripoti
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) siku moja kabla (Machi 18
mwaka huu).
Washiriki hao
ni makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na
Zanzibar. Pia waratibu wa mikoa wa mashindano ya Umoja wa Michezo wa
Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).
Barua za mwaliko kwa ajili ya semina hiyo tayari zimetumwa kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment