Thursday, March 14, 2013

PINDA MGENI RASMI TAMASHA LA PASAKA DAR ES SALAAM


Na Francis Dande

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha
la Pasaka Machi 31 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari  iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama tayari Ofisi ya Waziri Mkuu imeshathibitisha kuhusiana na ujio wake kwenye tamasha hilo.

“Tunafurahi kwamba tamasha letu mwaka huu Dar es Salaam mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mwaka jana alikuwa Waziri wa Mambo
ya Nje, Benard Membe,” ilisema taarifa hiyo ya Msama.

Waimbaji mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa kutumbuiza kwenye tamasha hilo, ambapo wan je ya nchi ni Sipho Makhabane wa Afrika Kusini, Ephraim Sekeleti wa Zambia na Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya, pamoja na kwaya ya Ambassadors of Christ ya Kigali Rwanda.

Kwa upande wa wasanii wa hapa nchini watakaotumbuiza ni Upendo Kilahiro,  Rose Muhando, Upendo Nkone na John Lissu, kwaya ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration.

Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam Machi 31 na  litaendelea Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati Aprili 3 ni Uwanja wa Samora Iringa na Aprili 6 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mbali ya tamasha hilo kuwa na malengo ya kueneza ujumbe wa neno la Mungu kupitia uimbaji, pia sehemu ya fedha amnbazo hutokana na viingilio hutumika kuwafariji walemavu, yatima na wajane.

Hata hivyo, kwa mwaka huu litatumika kufikisha ujumbe wa kusisitiza suala la amani na upendo kwa watu wote bila kujali dini, itikadi, jinsia wala rangi kwani wote ni wamoja mbele za Mwenyezi Mungu.

No comments:

Post a Comment