Monday, March 4, 2013

UCHAGUZI KENYA; KENYATA AZIDI KUMBURUZA ODINGA


Matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu nchini Kenya yanaonyesha kuwa Uhuru Kenyatta, mtoto wa Rais wa Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta anaongoza, huku akifuatiwa kwa karibu na aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Raila Odinga.
Kama alivyo Uhuru, Raila pia ni mtoto wa mmoja wa waasisi wa taifa la Kenya, ambaye alikuwa Makamu wa Mzee Kenyatta, Jaramong Oginga Odinga.
Hadi majira haya ya  saa 12.17 alfajiri ya leo,  Uhuru ambaye ni mgombea wa TNA alikuwa amepata kura 1,617,701 sawa na asilimia 54.79 wakati Raila ambaye ni mgombea wa ODM alikuwa akifuatia kwa kupata kura 1,201,910 sawa na asilimia 40.68.
Matokeo hayo ni kutoka katika vituo zaidi ya 8,300 kati ya 31,000 na yalikuwa yakionyeshwa moja kwa moja na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kadri yalivyokuwa yanaingia.
Hata hivyo Mwenyekiti wa IEBC, Isaack Hassan akizungumza na vyombo vya habari jana usiku alisema matokeo hayo ni ya awali na kwamba matokeo kamili yangetangazwa na tume yake baada ya kukusanya taarifa kutoka vituo vyote vya kupigia kura.
Wagombea wengine walikuwa wameachwa mbali. Hao ni Musalia Mudavadi, Peter Kenneth, James Kiyiapi, Martha Karua, Mohamed Dida na  Paul Muite.

No comments:

Post a Comment