Monday, March 4, 2013

SHULE YAITAJI MSAADA:INA WALIMU 8 SITA KATI YAO NI WAJAWAZITO

SERIKALI imeombwa iwapatie walimu wa kiume Shule ya Msingi Orbili, kutokana na walimu wote wanawake wa shule hiyo kupata ujauzito na hawafundishi hivi sasa.

Ombi hilo limetolewa na wakazi wa Kijiji cha Orbili Kata ya Shambarai wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Wakazi hao ambao hawakutaka kutaja majina yao wakati wakiongea na waandishi wa habari, walisema kuwa shule hiyo ina walimu nane, ambapo wanaume ni wawili na wanawake ni sita, akiwemo Mwalimu Mkuu, wote wana ujauzito.

Walisema walimu wawili wanaume, hawawezi kuwafundisha wanafunzi wote wa shule hiyo kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, hasa ukizingatia kuwa darasa la nne na la saba, watafanya mtihani wa Taifa mwaka huu.

Walisema kuwa hivi karibuni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, alijifungua mtoto na walimu wengine watano waliobaki, wanatarajiwa kujifungua wakati wowote.

Nadhani shule hii ifungwe ili Serikali ilete walimu wengine kwani hawa walimu wenye mimba hawafundishi wanafunzi wetu, wenyewe wamebaki kula udongo na malimao,” alisisitiza mkazi mmoja.


Imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la HabariLeo


No comments:

Post a Comment