Monday, March 11, 2013

SHERIA YA USHURU YAFUTWA MKOANI MBEYA

Imeandikwa na GORDON KALULUNGA, Mbeya

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya limelazimika kuifuta Sheria ndogo ya Halmashauri hiyo namba 376 (4) na (1) ya Mwaka 2011 iliyokuwa inataka kusajili magali ya kukodi, teksi,Bajaji na Pikipiki kwa kulipia ushuru Shilingi 58,000/= kwa Mwaka.

Sheria hiyo imefutwa baada ya kutokea maelewano hasi baina ya wamiliki na madereva wa magari kuanzia tani moja hadi tani nne na wakala aliyepewa zabuni ya kukusanya ushuru huo.

Ushuru unaolalamikiwa na wamiliki hao wa magari ni ule unaokusanywa na Halmashauri hiyo kupitia kwa wakala aliyejulikana kwa jina la Mbuzax Auction Mart & Court Brockers inayomilikiwa na Emmanuel Mbuza.

Wananchi hao walitoa malalamiko hayo kwenye mkutano wapamoja kati ya wamiliki wa magari, madereva na viongozi wa Halmashauri ya Jiji chini ya Meya uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri uliopo Sokomatola, Jijini hapa.

  • Dereva Paulo Mwasilelwa ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Waendesha malori wa Jiji la Mbeya alisema wanapingana na ushuru huo ambao unawaumiza kwa sababu hulazimika kulipia gharama za usajili wa gari linaponunuliwa, bima ya gari, TRA, maegesho na zimamoto na hivyo kudumaza uchumi wa mwananchi wa kawaida. Pia waliulalamikia utaratibu mbovu unaofanywa na wakala huyo ambao walidai akala hutumia nguvu nyingi kama vile mapanga ili kuwatisha na hata kuwajeruhi madereva na hivyo kuhatarisha maisha yao. “Msheshimiwa meya huyu wakala anatumia mabavu kukusanya ushuru wake ambapo hadi sasa kuna watu wamejeruhiwa na mapanga lakini pia anakusanya hata kwenye magari ambayo hayafanyi biashara ndani ya Jiji huku mengine yakiwa yanapita tu.” alisema Katibu huyo.
  • Akijibu tuhuma hizo, Meya wa Jiji la Mbeya bwana Attanas Kapunga aliyekuwa amefuatana na Kamati ya Fedha ya baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo alisema kutokana na sheria iliyokuwa imepitishwa na madiwani hao kutotolewa elimu kwa wananchi wanaotakiwa kulipa kodi inamakosa. “Halmashauri imefanya makosa kutowapa elimu walipa kodi lakini pia wakala anamakosa makubwa kwa sababu sheria inataka magari yanayofanya biashara ndani ya Halmashauri ndiyo yalipe ushuru na si vinginevyo,” alisema Meya.
  • Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Mbuzax ndugu Emmanuel Mbuza ambaye awali hakupewa nafasi ya kujitetea kutokana na madereva kumzomea pindi aliponyoosha mkono akitaka kujitetea hadi mkutano unafungwa aliwaambia waandishi wa habari kuwa anaishukuru Halmashauri hiyo kwa kugundua mapungufu ya sheria zao ambazo sasa kufutwa kwake kutampunguzia kufanya kazi katika mazingira magumu yanayosababisha kuwa na ugomvi na wananchi.

Soma habari kamili kwenye blog ya Kalulunga

No comments:

Post a Comment