Friday, March 15, 2013

MKUU WA WILAYA AMUONDOA MKURUGENZI WA MAJI IGUNGA


ig11MKUU wa Wilaya ya Igunga, Tabora Elibariki Kingu, amemuondoa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka na kumrejesha kwa Mwajili wake kutokana na kushindwa kwake kusimamia Mradi wa maji katika Bwawa la Bulenya.
 Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kingu alisema alikwisha mwandikia barua  Mkurugenzi huyo, Lema Jeremia, ambapo alisisitiza kuwa barua hiyo si ya kumfukuza kazi bali ni ya kumuondoa wilayani kwake.
 “Kazi hii alipewa Mkandarasi anayeitwa Wessons Tanzania Limited, mradi huu ulikuwa ni lot No. IG14 na mkataba namba IDC/CF/T/04/05/29, ambapo mkataba ulisainiwa Julai 29, 2008 huku muda wa utekelezaji ukiwa ni miezi sita lakini hadi leo ni miaka mitano mradi huo haujakamilika”alisema Kingu.
 
Alisema mkurugenzi huyo alifumbia macho matatizo ya maji katika wilaya hiyo, kusababisha Serikali ishindwe kutimiza ahadi zake kikamilifu kwa wananchi na kwa makusudi alisaini cheki za malipo wakati akitambua wazi hakuna mradi uliokamilika.
 
Kingu alisema  mradi huo uliotengewa sh bilioni 1.94 kwa ajili ya kuengeneza miundombinu ya vituo vya kusambaza maji katika wilaya hiyo.
 
Alisema mradi huo ulitarajiwa kukamilika Januari 2009, cha kushangaza hadi mwaka huu wa 2013, mkandarasi amelipwa zaidi ya asilimia 95 ya fedha ambazo ni sh milioni 9.7 huku akiwa hajakabidhi kazi.
 
“Baada ya uamuzi huo, nimeviagiza vyombo vya dola hususan Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kukamilisha haraka uchunguzi na kumfungulia mashitaka mara moja”alisema Kingu
 
Kingu alibainisha kuwa vituo tisa kati ya 13 ambavyo vilipaswa kutoa maji vimetelekezwa na havitoi maji ambapo alivitaja kuwa ni NMB, Kwa Mzee Costa,Masanga, CCM, Kilabu cha China, Kamando, Kokoto, Mwayunge na Mnadani.
 
“Hili nitalifanyia kazi na wala sitamuogopa mwananasiasa yeyote hata kama ni kupoteza kazi niko tayari, lakini siko tayari kufukuzwa kazi kwa ajili ya uzembe wa mtu mwingine anayeshindwa kutimiza majukumu yake, kwa ajili ya manufaa ya wananchi”alisema Kingu.
 
Alipotafutwa Jeremia, ili kutoa ufafanuzi kuhusu kauli ya Mkuu wa Wailaya huyo, alikiri kupokea barua hiyo hata hivyo, alisema kuchelewa kwa mradi huo kunatokana na mwaajili wake kuchelewa kulipa fedha za mradi huo kwa wakati.
 Vilevile alisema hakuna fedha zilizolipwa nje ya kazi, amabapo pia alidai kuwa mradi huo hadi sasa umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.

No comments:

Post a Comment