Tuesday, March 5, 2013

MALI YA SERIKALI YENYE THAMANI YA MILIONI 300 YAUZWA KWA MILIONI 2.5

Picture
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balopzi Seif Iddi, akiangalia waya wa umeme aina ya shaba ambao amezuia mauzo yake hadi uongozi wa kiwanda cha sukari utapokaa pamoja na Wizara ya fedha kufikia maamuzi, kutokana na waya huo kuuzwa chini ya thamani na baadhi ya maafisa wa Serikali. Thamani halisi ya waya huo inakadiriwa kuwa ni Tsh 300 millioni lakini umeuzwa kwa Tsh 2.5 millioni tu.
Tukio hilo limebainika mara baada ya Makamu huyo kutembelea kwenye kiwanda cha Sukari kilichopo Mahonda mjini Zanzibar na kuzungumza na uongozi wa kiwanda hicho ambacho kiliuziwa waya huo kwa bei ya chee.

Balozi Seif alisema zipo hitilafu zinazotumiwa na baadhi ya maafisa wa Serikali katika mauzo ya mali za Serikali na matokeo yake kusababisha kuitia hasara kubwa Serikali Kuu.

Amesema mali za Serikali zimekuwa zikinunuliwa kwa gharama kubwa lakini uuzwaji wake baada ya matumizi hayalingani na thamani ya mali zenyewe jambo ambalo hutoa mwanya kwa mali hizo kuuzwa kwa bei ya chini kabisa.

Utashangaa kuona mali za Serikali hununuliwa kwa gharama kubwa lakini baadhi ya maafisa na watendaji wa serikali hutumia mwanya wa kujenga hoja ya kuuzwa mali hizo kwa kisingizio cha kuchakaa na badala yake baadhi yao kujiuzia wenyewe kwa bei wanayoitaka wao wenyewe bila ya kuzingatia taratibu zilizopo za tenda na mnada”. alionya Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kukaa pamoja na Uongozi wa Kiwanda cha Sukari kuangalia nanma ya matumizi ya waya huo ambao ulikuwa ukitumiwa na Kiwanda hicho.

Waya huo ulilazimika kufukuliwa na Uongozi wa Kiwanda hicho baada ya kubainika kuanza kuhujumiwa kwa kukatwa katwa na baadhi ya wezi kufuatia kutambulikana thamani yake katika masoko ya Kimataifa.   

Mapema Mshauri wa Kiwanda cha Sukari Mahonda, Dk Hamza Hussein Sabri alisema Zanzibar inatarajiwa kujitosheleza kwa sukari ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu kufuatia uongozi wa kiwanda cha sukari cha Mahonda kufanikiwa kupata washirika zaidi katika kuongeza nguvu ya kuanza uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa jamii.

via SaidPowa blog

No comments:

Post a Comment