Saturday, March 9, 2013

JK AMTUMIA SALAMU ZA PONGEZI RAIS MTEULE WA KENYA UHURU KENYATTA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jayaka Mrisho Kikwete amemtumia salamu za pongezi nyingi Rais Mteule wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta.

Katika salamu hizo zilizotumwa leo, Jumamosi, Machi 9, 2013, saa chache baada ya kuthibitishwa rasmi kuwa Mheshimiwa Kenyatta ameshinda Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika mwanzoni mwa wiki hii Jumatatu, Machi 4, 2013, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Uhuru Kenyatta:

“Mpendwa Rais Mteule na Kaka, ilikuwa ni furaha kubwa kwangu kupokea taarifa ya ushindi wako wa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya. Niruhusu, kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania, na kwa hakika, kwa niaba yangu binafsi kukupogenza kwa dhati ya moyo wangu kwa mafanikio haya makubwa ya kuchaguliwa kwako.”

Ameongeza Rais Kikwete: “ Ushindi huu ni ushahidi na ishara ya wazi kabisa ya imani na matumaini ambayo wananchi wa Kenya waliyonayo katika uongozi wako. Huu ni utambuzi wa kazi yako maridadi na mchango wako mkubwa ambao umeutoa katika nafasi mbali mbali za uongozi katika siku za nyuma katika jitihada zako za kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ustawi wa nchi yako na wananchi wake.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Wakati unajiandaa kuchukua madaraka ya juu zaidi katika nchi yako, napenda kukuhakikishia msimamo wake binafsi pamoja na ule wa Serikali yangu wa kuunga mkono Serikali yako. Ni imani yangu kubwa kwamba pamoja tutaweza kuendelea kusukuma mbele zaidi maendeleo ya nchi zetu – Kenya na Tanzania na pia utengamano wa Afrika Mashariki kwa manufaa ya nchi zetu na wananchi wake.”

No comments:

Post a Comment