Sunday, March 10, 2013

BINGWA WA KARATE DUNIANI KUREKODI FILAMU YA ALBINO TANZANIA


Na Mwandishi wetu
KAMPUNI ya  Advanced security Limited imeingia  makubaliano na bingwa wa dunia wa mchezo wa Kareti,  Profesa Maurizio Martina wa Italia kwa ajili ya kutengeneza filamu mbalimbali pamoja na ile inayopinga mauaji ya walemavu wa ngozi, albino na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake.

Makubaliano hayo yalifanyika jana kwenye hotel ya JB Delmonte na filamu hiyo itaanza kurekodiwa ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa na kukamilika kwa miezi mitatu.

Mwenyekiti wa Kampuni ya Advanced Security Limited, Juma Ndambile alisema kuwa  sababu kubwa ya kuingia katika masuala ya filamu ni moja ya shughuli zake katika kujihusisha na masuala ya jamii.

Ndambile alisema kuwa kampuni yao ni Limited na kutokana na hilo inaweza kufanya shughuli nyingine mbalimbali tofauti na huduma ya ulinzi na usalama.

Alisema kuwa katika filamu hiyo, atawashirikisha waigizaji mbali mbali wa hapa nyumbani na wapo mbioni kukamilisha taratibu zote kwa mujibu wa sheria ya kurekodi filamu hapa nchini.


Kwa mujibu wa Ndambile, Profesa  Maurizio  ambaye ameigiza filamu nyingi katika nchi za mbali mbali pamoja na Uingereza na Marekani mbali ya Italia atashirikiana na mke wake, Angel Howel na mwanaye, Dumiano ambaye amewahi kuigiza na mcheza filamu maarufu duniani.

Profesa Maurizio alisema kuwa pia atafundisha wanawake jinsi ya kujilinda kwa kutumia mchezo wa karate ili kuondoa unyanyasaji wa wanawake nchini.

Amesema kuwa amefanya kazi  hiyo nchi mbali mbali ikiwa pamoja na DR Congo na Afrika Kusini.

“Lengo la filamu yangu ni kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na mila potofu za kuwaangamiza albino na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake,” alisema Profesa Maurizio ambaye pia ni Rais wa Dunia wa Shirikisho la Mchezo wa Kareti.

Maelezo ya picha

Bingwa wa Dunia wa mchezo wa Karate ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la mchezo huo duniani, Professa Maurizio Martina akionyesha moja ya mbinu atakazozitumia kuwafundisha albino na wanawake kwa lengo la kujilinda wakati wa mkutano na waandishi wa habari jana uliofanyika kwenye hotel ya JB Delmonte.

No comments:

Post a Comment