JOPO la Madaktari wa Chuo wa Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili (MUHAS), limekamilisha utafiti wa chanjo mpya ya
virusi vya Ukimwi, ambao umethibitisha kuwa chanjo ya DNA -MVA ilikuwa
salama na yenye uwezo wa kufanya mwili utengeneze kinga dhidi ya virusi
vya Ukimwi (VVU).
Utafiti huo ulifanyika nchini kati ya mwaka 2007-2010 na 2008-2012.
Utafiti wa awali uliofanyika kati ya mwaka 2007
hadi 2010, ambao ulijulikana kama HIVIS-03, ulihusisha askari 60 polisi
na magereza wa jijini Dar es Salaam, ambao walipewa chanjo hiyo na
baadaye kuachwa wakiishi maisha yao ya kawaida kwa muda wa miaka mitano.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Profesa
Muhammad Bakari, aliyeongoza jopo la madaktari waliofanya utafiti huo
alisema kuwa umezaa matunda na kuthibitisha kwamba chanjo ya DNA –MVA
waliyopewa askari hao, ilikuwa salama na yenye uwezo wa kufanya mwili
utengeneze kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi (VVU).
“Chanjo hiyo inaweza kutengeneza vichocheo vya
kinga dhidi ya VVU kwa asilimia 100 kwa washiriki waliopatiwa chanjo
zote tano. Haya ni matokeo mazuri sana kupita hata matarajio watafiti,
pia ni ya muhimu katika harakati za kutafuta chanjo dhidi ya VVU,”
alisema.
Profesa Bakari, ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Mafunzo wa MUHAS, alisema kwamba hakuna mshiriki aliyekufa, wala kupata
athari za moja kwa moja kwa na kupatiwa chanjo kutokana na tafiti hizo.
Alisema kuwa askari walioshiriki utafiti huo walifanya hivyo kwa hiari yao hadi kukamilisha utafiti huo.
Alibainisha kwamba jopo la madaktari bado
liliendelea na utafiti zaidi, ulioanza mwaka 2008 hadi 2012, ili kupata
chanjo sahihi ya VVU kwa aina ya pili ya chanjo ijulikanayo kama
TAMOVAC-01(Tanzania and Mozambique HIV Vaccine Program), iliyohusisha
pia nchi ya Msumbiji.
“Hatukuishi hapo, utafiti wa pili (TAMOVAC-01),
ulifanyika kati ya mwaka 2008 na mwaka 2012. Utafiti huu ulijumuisha pia
nchi ya Msumbiji.
Profesa Bakari alisema kuwa utafiti nchini Tanzania ulihusisha washiriki 120, kati yao 60 wakiwa ni kutoka jijini Dar es Salaam.
Alibainisha kwamba kwa mara nyingine washiriki hao
walitoka katika Jeshi la Polisi, Magereza na raia wa kawaida, huku
wengine 60 wakiwa raia wa kawaida kutoka jijini Mbeya.
Mtaalamu huyo alieleza kwamba utafiti huo pia ulionyesha kuwa mchanganyiko wa chanjo ya DNA-MVA ulikuwa salama.Mwananchi.
No comments:
Post a Comment