Na Willbroad Mathias, Majira, Dar es Salaam -- JESHI
la Polisi Kikosi cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, kinawashikilia
Watanzania wawili waishio nchini Afrika Kusini baada ya kukamatwa wakiwa
na euro bandia zenye thamani inayokadiliwa kufikia sh. milioni 10.
Vyanzo
vyetu vya habari vimedai kuwa, watuhumiwa hao ni mwanamke na mwanaume
ambao walikamatwa juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu
Julius Nyerere (JKNIA), Dar es Salaam.
Inadaiwa kuwa, kabla ya
kukamatwa ulitokea mvutano kati ya mtuhumiwa mwanamke na mwenzake ambaye
waliambatana katika uwanja huo wakati mtuhumiwa mwanaume akiwa
ndani. Hali hiyo iliwafanya polisi kuingiwa na shaka hivyo walianza
kufuatilia kile kinachobishaniwa.
“Kabla ya kuwakamata
watuhumiwa, ulitokea mvutano wakati huo mtuhumiwa wa kiume alikuwa
katika chumba cha mapumziko tayari kwa safari ya kwenda nchini Afrika
Kusini. Baada ya polisi kubaini chanzo cha mabishano hayo, waliamua
kumsaka mtuhumiwa wa kiume na kumfanyia upekuzi upya ndipo alipokutwa na
euro bandia,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliongeza
kuwa, mbali ya kukamatwa na Euro hizo mtuhumiwa huyo pia alikutwa na
fedha nyingine za Kitanzania zinazokaribia kufikia sh. milioni tatu
pamoja na hati mbili za kusafiria moja ya Tanzania na nyingine Afrika
Kusini.
Akithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Kamishna Mkuu
wa Kikosi hicho, Kamanda Ulrich Matei, alisema walikamatwa saa tisa
alasiri na kuwataja majina yao kuwa ni Bw. Omary Salum na Bi. Khadja
Yusuf, ambao wanaishi nchini Afrika Kusini. Alisema kwa mujibu wa
maelezo ya Bw. Salum, alikuja ili kununua dhahabu na kopa mjini Songea,
mkoani Ruvuma, lakini baada ya kufika mkoani humo alikuta biashara ni
ngumu akaamua kuondoka. Aliongeza kuwa, Salum baada ya kufika Dar es
Salaam, alikuwa apokelewe na Bi. Yusuf, ambaye kwa sasa yupo Tanzania
lakini anaishi nchini humo. Hata hivyo, Kamishna Matei alisema baada ya
kuhojiwa, Bw. Salum alidai fedha hizo alibadilishana na raia mmoja wa
China ambapo yeye alimpatia randi 70,000 na kupewa kiasi hicho cha
fedha.
Akizungumzia mazingira yaliyosabisha kukamatwa kake,
Kamanda Matei alisema siku ya tukio Bw. Salum alikuwa akutane na Bi.
Yusuf, uwanjani hapo, “Bw. Salum alipofika uwanja wa ndege, mwenyeji
wake Bi. Yusuf alikuwa amechelewa, muda wote walikuwa wakiwasiliana kwa
simu ya ofisa wetu mmoja kwani mtuhumiwa hakuwa na laini ya simu za
Tanzania,” alisema Kamanda Matei na kwamba baada ya muda mfupi, Bi.
Yusuf aliwasiri uwanjani hapo akiwa na mwanamke mwingine aliyemtaja kwa
jina la Bi. Zamzam Shaban.
Bi. Shaban aliuliza alipo Salum na
baada ya kuambiwa tayari ameingia ndani, alianza kulalama na kudai
mtuhumiwa alikuwa mpenzi wake na walikubaliana ampe pesa badala yake
amemtoroka hivyo aliamua kutoa siri ya mtuhumiwa kufanya biashara ya
kuuza noti bandia.
Alisema hivi sasa wanamshikilia Bi. Yusuf kwa
sababu baada ya Bi. Shaban kutoa siri hiyo, alituma ujumbe mfupi (sms),
kumjulisha Bw. Salum kuwa atafute njia ya kujinusuru.
Ujumbe huo
ulitumwa katika simu ya ofisa huyo baada ya Bi. Yusuf kudhani kuwa, simu
hiyo ilikuwa ya mtuhumiwa ambapo kazi ya kumsaka Bw. Salum, ilianza na
kukamatwa.