Saturday, September 1, 2012

WASIMAMIZI WA TRENI ZA ABIRIA WATAKIWA KUHARAKISHA KUTENGENEZA MABEHEWA ILI TRENI ZA ABIRIA ZIJARIIWE SEPTEMBER 10, 2012

Hapa naibu waziri wa uchukuzi Dk Charles Tizeba akiwa na viongozi wengine picha hii ni kwahisani ya Mtandao

NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Charles Tizeba ameuagiza uongozi unaosimamia mradi wa kutengeneza mabehewa ya treni kwa ajili ya usafiri jijini Dar es Salaam, kukamilisha kazi hiyo kabla ya Septemba, 10, mwaka huu, ili mabehewa hayo yafanyiwe majaribio.

Kukamilika kwa mabehewa, itakuwa ni hatua ya kwanza kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, kuanza kutumia usafiri wa treni, ili kupunguza msongamano wa foleni.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, baada ya kufanya ziara ya kushitukiza ya kukagua mabehewa kwenye karakana ya Shirika la Reli Tanzania (TRL), Dkt. Tizeba alisema, ameridhishwa na kasi na kiwango cha utengenezaji wa mabehewa hayo, licha ya kuwepo changamoto mbalimbali, “Tumekubaliana ifikapo Septemba 10, mwaka huu tutafanya majaribio ya treni hizi, kutoka katikati ya Jiji kwenda Ubungo, ili kuangalia kama yana uwezo mzuri wa kubeba abiria,” alisema Tizeba.

Katika karakana ya TRL mabehewa 9 yapo katika hatua za mwisho za ukarabati huku hali katika karakana ya TAZARA ikiwa hairidhishi.

Akizungumza na mafundi wa mabehewa hayo TRL, Dkt. Tizeba aliwataka kuhakikisha kwamba mabehewa hayo yanakamilika kwa ajili ya kuanza kutoa huduma ifikapo Oktoba mwaka huu, “Kuanzia leo nawapa siku 10 treni za majaribio ziwe tayari, na nitazungumza na wanaohusika na reli wahakikishe hadi Septemba nane mwaka huu njia hizo ziwe zinapitika,” alisema.

Kwa upande wa TAZARA, naibu Waziri huyo alionekana kutoridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa hadi sasa bado hakuna behewa ambalo linakaribia kumalizika huku wafanyakazi wake wakidai wameshalipwa posho ya mwezi mzima uliopita. “Hivi kweli hii ndiyo kazi mnanieleza mmefanya kwa mwezi huu mzima?

Kazi hii hairidhishi na hali ni mbaya sana, kwa kweli spidi hii ya ukarabati wa mabehewa si nzuri na inatakiwa iendane na matarajio,” alisema.

Hata hivyo alipendekeza viti vya mabehewa hayo viwe vya plastiki kama vilivyo uwanja wa taifa, badala ya vya sponji walivyoviweka kwa kuwa itakuwa ni rahisi kuharibika na kuhifadhi uchafu. 

Pia alitaka mamlaka husika kuhakikisha wanaandaa utaratibu wa kukata tiketi kwa mashine ili kudhibiti ubadhirifu badala ya ilivyopendekezwa sasa ya kuwepo na watu wawili watakaokuwa wakipokea fedha mlangoni.

Wakizungumzia changamoto zinazowakabili, wafanyakazi wa karakana ya TRL, Juma Humelezi na Kapaya Juma walisema kuwa hawana vitendea kazi na posho wanazopata ni ndogo ikilinganishwa na ugumu wa kazi.

Wafanyakazi hao wamekuwa wakidai nyongeza ya posho hadi Sh 10,000 kwa kuwa Sh 5,000 ambayo wamekuwa wakilipwa kwa sasa haiwatoshi huku wenzao wa TRL wao wakipokea posho ya Sh 2,500, “Tukiongezwa posho na kazi inachangamka kwa kuwa tunakuwa na nguvu za kutosha ila kwa sasa posho ni ndogo wakati kazi ni ngumu na kuna wenzetu wapo kwenye rangi nao wanahitajika kupata maziwa kwa kuwa wanacheza na sumu,” walisema.

Kuhusu malalamiko hayo, Dkt. Tizeba alisema siku zote hakuna anayetosheka na fedha, hivyo amewataka wafanye kulingana na makubaliano.

Naye msimamizi mkuu wa maradi huo, Ibrahim Kapenta alisema, karakana hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kufanyia kazi ambavyo huwasaidia wafanyakazi kujikinga na magonjwa ya kuambukiza. Alisema hadi sasa, mabehewa ambayo yanamwelekeo mzuri ni tisa, wakati mabehewa sita ndiyo yanayotarajiwa kufanyiwa majaribio.

Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kumaliza tatizo la foleni jijini Dar es Salaam ambapo treni moja itakuwa ikichukua abiria zaidi ya 240 kwa safari moja na njia za kuanzia itakuwa ni Mwakanga hadi bandarini na Ubungo Maziwa hadi Stesheni.