Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imemsimamisha kazi na itamchukulia
hatua za kinidhamu Mkuu wa Idara ya Utafiti, Tathmini na Huduma za
Kompyuta, Joseph Mbowe baada ya uchunguzi kubaini kuwapo kwa dosari
katika ukokotoaji wa alama za mitihani ya somo la Islamic Knowledge
katika kompyuta.
Aidha,
Wizara hiyo imeagiza NECTA kukokotoa upya alama za mitihani ya
wanafunzi wa kidato cha sita ya somo hilo waliofelishwa kwa bahati mbaya
mwaka huu kutokana na dosari hiyo na tayari matokeo ya alama hizo
yametolewa.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo na Ufundi, Philip Mulugo alisema Mei 28, mwaka huu, Wizara
ilipokea malalamiko kutoka Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislamu, dhidi
ya matokeo ya wanafunzi wa kidato cha sita mwaka huu katika somo hilo.
Alisema
baada ya Serikali kupokea malalamiko hayo iliunda tume ya watu tisa
ikijumuisha wajumbe kutoka Wizara ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Wizara ya Elimu na Amali Zanzibar, Necta, Baraza la Elimu la
Kiislamu, Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislamu, Idara ya Usalama wa
Taifa na Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Alisema
kamati hiyo ilitakiwa kupitia orodha ya wasahihishaji wa somo hilo,
kupitia maoni ya wasahihishaji, sampuli za mitihani za watahiniwa,
kuhakiki uhamishaji wa alama kutoka mitihani kwenda kwenye kompyuta na
kulinganisha mchakato wa usahihishaji na matokeo ya somo hilo kwa mwaka
huu na miaka ya nyuma.
Mulugo
alibainisha kuwa baada ya uchunguzi wa kamati hiyo ilibaini kuwa
ukokotoaji wa alama za mitihani ya somo hilo ulikuwa na dosari kutokana
na mfumo uliotumika kukokotolea kutofanyiwa marekebisho kulingana na
mabadiliko ya sasa.
“Miaka
ya nyuma somo hili lilikuwa linafanywa mitihani mitatu ambapo mfumo wa
kompyuta ulikuwa unakokotoa na kugawanya alama kwa kutumia idadi hiyo ya
mitihani mitatu, lakini mwaka huu tumebadilisha na mitihani ya somo
hili ni miwili, lakini ukokotoaji uliotumika ni wa zamani wa kugawanya
kwa mitihani mitatu,” alisema.
Alisema
baada ya matokeo hayo, Serikali imeagiza Necta imchukulie hatua za
kinidhamu Mbowe ambapo pia tayari wanafunzi waliofelishwa kutokana na
dosari hiyo, alama zao za mitihani zimekokotolewa upya kwa mfumo wa
sasa.
Sakata la
kufeli kwa wanafunzi wa somo hilo mwaka huu, liliibua mjadala mkubwa
ambapo Jumuiya na taasisi za Kiislamu zilifikia hatua ya kutaka
Mkurugenzi Mtendaji wa Necta, Dk Ndalichako na Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa wajiuzulu kutokana na uzembe
uliotokea.