KATIKA hali ya kustaajabisha wananchi na hata wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, mkazi wa Kijiji cha Kingerikiti, Kata ya
Kingerikiti, wilayani hapa, Jackson Mbunda (35), ameitaka Katiba mpya
iruhusu uvutaji bangi nchini.
Amesema,
maoni yake hayo yanazingatia ukweli kwamba, bangi ni aina mojawapo ya
tumbaku na kiburudisho na anashangaa kwa nini sigara imeruhusiwa lakini
bangi imepigwa marufuku.
Akitoa
maoni yake jana, katika Kata ya Kingerikiti mbele ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Mbunda alisema, “Napendekeza kuwa bangi iruhusiwe kwa vijana
lakini iwekewe maelezo kama yalio kwenye sigara.”
Mbunda
akisimamia maoni yake hayo yaliyosababisha miguno kwa wananchi
waliohudhuria mkutano huo na hata baadhi ya wajumbe wa Tume, alisema
sababu ya kupendekeza hayo ni kutokana na hali halisi kuwa vijana
wanazidi kuharibika kwa kuwa wanavutia uchochoroni.
“Nashangaa
kwa nini sigara inaruhusiwa lakini bangi inapigwa vita, sijui kama
serikali inafahamu kuwa vijana wengi wanavuta bangi kwa makosa huko
vijiweni na uchochoroni, hawa wangewekewa maelekezo ya namna ya kuvuta
bangi na ikawa ruksa, wasingeharibika kama ilivyo sasa,” alisisitiza
Mbunda.
Alisema mpaka
sasa takwimu za vijana wanaoharibika kwa bangi na dawa nyingine za
kulevya ni wengi lakini ikiwa itaruhusiwa kisheria na kuwapa vijana
maelekezo ya namna ya kutumia, wataweza kufanya kazi na kuingiza kipato
badala ya muda mwingi kuutumia kwenye vificho.
Hata hivyo, Wajumbe wa Tume hawakumuuliza ufafanuzi wowote kama ilivyo kawaida.
Awali, Mwenyekiti wa msafara ulioko mkoani Ruvuma, Profesa Mwesiga Baregu aliwataka watoe maoni bila wasiwasi wowote.