Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa taarifa usiku wa jana
ikieleza idadi ya watu waliopatikana wakiwa hai ni 146 na kupata maiti 62.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari ,Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamuhuna alisema taarifa hiyo
ndio sahihi na kuwataka wananchi kutoamini taarifa zinazotolewa na watu wengine
zaidi ya Serikali.
Waziri Shamuhuna alisema kwamba maiti 62 walipatikana
ambao kati ya maiti hizo watoto ni 9 na kuna raia mmoja wa kike wa kigeni
ambaye hakuweza kutambulika Uraia wake,lakini imeonekana picha yake moja
ndogo ya hati ya kusafiria.
Waziri Shamuhuna alisema meli hiyo ilibeba jumla ya
abiria 290 kati ya hao watu wazima 250, watoto wadogo 31 na mabaharia 9.
Waziri huyo aliwataka wananchi katika sehemu mbalimbali
hasa katika vijiji vilivyo kandokando ya bahari watakapoona maiti au mtu akiwa
hai ambaye wanadhani ni wa ajali ya Meli ya Skagit.
Aidha, Waziri Shamuhuna alisema kwamba kwa wakazi wa Jiji
la Dar es Salaam ambao watakuwa na wasiwasi wa kutowaona ndugu na jamaa zao
amewataka kufika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kupata
taarifa zaidi au kuripoti habari za kupotelewa kwa ndugu au jamaa zao.
Kwa upande wa Zanzibar, Waziri huyo aliwataka wananchi
kufika kwa Masheha wao kutoa taarifa kama hizo.
Serikali imewashukuru makampuni binafsi za usafiri
baharini kwa msaada wao na wasisite kutoa msaada katika kazi inayoendelea ya
kutafuta watu au maiti wengine katika eneo la tukio.
Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 karibu na Kisiwa
cha Chumbe umbali wa maili sita kuelekea Kusini mwa Kisiwa kidogo cha Yasin
Zanzibar ikitokea Bandari ya Dar es Salaam ilikoanza safari saa 5:30 asubuhi.
Meli hiyo inamilikiwa na Kampuni ya Sea Guall Sea
Transport Ltd, Kampuni ambayo Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilizama ikiwa
Bandarini Malindi Zanzibar na kufariki watu sita mwaka 2009.
Mwisho.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR
ZANZIBAR, TANZANIA
JULAI 19,2012