Kutokana na
tukio la vifo vya watu waliokunywa Pombe kali ya Gongo hivi karibuni, mimi
binafsi napenda kuwaletea picha chache tu kuonyesha namna pombe hiyo
inavyoandaliwa.
Kule kwetu
Pombe hii huitwa kwa jina la NIPA wengine kwa kuipendezesha wakalirefusha jina
hilo kuwa "New Internationa Pure Alcohol" na kwa hakika viongozi
wengi waliotokana na makabila ya Wayao na Wamakuwa walisoma kutokana na ADA ya
mapato ya pombe hiyo kali. Itakumbukwa kuwa kwa mara ya kwanza katika kampeni
za uchaguzi za mwaka 1995 Mgombea moja alidiriki kuwaahidi wananchi wa makabila
hayo kuwa wakimchagua ataruhusu pombe hiyo na kuiwezesha iwe inaandaliwa
kitaalamu, ingawa kura hazikutosha.
Pombe ya
Gongo au Nipa kule kwetu hutokana na Mabibo (tunda la mkorosho) ambalo
hukaushwa juani na hatimaye kuweza kuhifadhiwa hata kwa zaidi ya miezi sita.
Mabibo unayoyasikia yakishakauka hubadilika jina na kuitwa KOCHOKO
ambazo inapofika wakati wake (ni baada ya msimu wa mauzo ya korosho
kupita) hupatikana kwa adimu sana na waandaaji wake huitafuta hata kwa maili
zaidi ya 60.
Kochoko hizo
baada ya kuchambuliwa na kuondoa takataka hulowekwa kwa wiki nzima ndani ya
pipa au mtungi (chungu kikubwa) na maji yake yakipata ladha ya juisi inayoweza
kulevya (staili ya mnazi au ulanzi), ndipo huwa tayari kwa kupikwa kama
unavyoona hizo picha.
Vifaa
vilivyosababisha jungu hilo ni: Mtungi, mtutu uliounganishwa na ngalawa, chungu
kidogo cha kufunika mtungi kwa ajili ya kuzua mvuke usitoke nje, udongo wa
mfinyanzi kwa ajili ya kusiliba maunganisho ya mtungi na chungu na tundu la
mtutu kutolea mvuke hadi kwenye chupa.
Mvuke
unaotoka hupozwa ndani ya mtutu kwa maji baridi na kuwa maji yanayoitwa NIPA
(Gongo). Ile Pure huitwa IPACHO ambayo ni Spiriti kabisa kwa kuwa inawaka
wanapoijaribia wenyewe, ile ya mwisho inaitwa ALEKA ambayo kwa wanaojifunza
huweza kuitumia. Ili kupunguza makali ya IPACHO huwa inachanganywa na ALEKA,
hata hapo Konyagi ni cha mtoto.