Chama cha wasanii
Tanzania (SHIWATA) imekubaliwa kupata kibali cha kuandaa mashindano ya ndondi
za kulipwa kupitia Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC) kwa kipindi cha
mwaka mmoja kuanzia Julai 24 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Viwango vya Mabondia wa Ngumi
za Kulipwa TPBC, Boniface Wambura alisema kibali hicho kinaruhusu
SHIWATA kuandaa mapambano na la kuanzia ni kati ya bondia Alfonce Joseph
(Mchumiatumbo) na David Michael Mlope (Zola D – King) litakalofanyika katika
Tamasha la Watani wa jadi katika Sikukuu ya Idd El Fitri kwenye Uwanja wa Chuo
cha Bandari Temeke.
Pambano hilo ambalo limeandaliwa na SHIWATA ili
kukusanya fedha za Ujenzi wa nyumba za kisasa za gharama nafuu kwa ajili ya
Wasanii, Waandishi wa Habari na Wanamichezo katika Kijiji cha Mwanzega,
Mkuranga.
Kamisheni ya Ngumi za kulipwa nchini Tanzania (TPBC)
ambalo inasimamia pambano hilo la Mabondia hawa watakaocheza katika uzani
wa juu (Heavy Weight) raundi nane (8) pia kutakuwa na pambano moja la
utangulizi.
Mwenyekiti wa SHIWATA Cassim Taalib alisema pamoja na
pambano hilo, kutakuwa na mechi ya mpira wa miguu kati ya Simba na Yanga
(Veteran) katika Uwanja huo huo wa Chuo cha Bandari Temeke na mshindi wa mchezo
huo atazawadiwa ng’ombe dume.
Taalib alisema kwamba kikundi cha Mchiriku cha Jagwa
kitatumbuiza, Roman Mg’ande wa Msondo atapigana mieleka na Lumole Matovolwa
(Big na upande wa wanawake Sophia Lubuva wa Simba atapambana na Mwajuma Jimama
wa Yanga huku washangiliaji wa Mpira Pesa (Simba) watapambana katika
mpira wa miguu na Watani wao wa jadi Yanga Bomba.
Tamasha litapambwa na mechi ya Mpira wa Kikapu ya
Ngongoti pamoja na mashindano ya Pikipiki ambayo yanatarajiwa kuwa kivutio
kikubwa kwa watoto na wakubwa ambao siku hiyo watakuwa wakisherekea Sikukuu ya
Idd el fitri baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani, Wasanii wa Bongo Flava
nao watakuwepo.
|