Sunday, July 22, 2012

MMILIKI PAMOJA NA NAHODHA WA MELI YA SKAGIT WAPELEKWA MBARONI, NAHODHA AELEZA JINSI ALIVYONUSURIKA KUFA, MAITI NYINGINE ZAPATIKANA.

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi-Zanzibar
Jeshi la Polisi kisiwani  Zanzibar, linawashikilia wafanyakazi sita wa meli ya MV Skagit akiwemo mmiliki wake Bw. Said
Abdulrahman pamoja na Nahodha wa meli hiyo Bw. Mussa Makame Mussa.wanahojiwa kuhusiana na tukio la ajali ya meli hiyoiliyosababisha vifo vya baadhi ya abiria  waliokuwa wakisafiri kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Bandari yaZanzibar.

Watuhumiwa hao walikuwa wakihojiwa katika Ofisi za Upelelezi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi mjini Zanzibar
ambapo Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, ACP Yusuph Ilembo, amesema watuhumiwa hao watafikishwa 
mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Kamanda Ilembo amesema kuwa Makachero wa Jeshi la Polisi wanaendelea na uchunguzi na kutafuta taarifa nyingine zinazohusiana na tukio hilo.

Hata hivyo, Nahodha wa zamu siku ya tukio hilo la kupinduka na kuzama kwa meli hiyo ya MV Skagit, Bw.Mussa Makame 
Mussa, ameelezea kwa ufupi jinsi ajali hiyo ilivyotokea na namna yeye alivyonusurika katika ajali hiyo.

Alisema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya kupigwa na dhoruba na mawimbi yaliyoambatana na upepo mkali, ambapo yeye alinusurika kufa maji baada ya kuruka kwa kutumia mlango wa mbele wa meli hiyo na kuanza kuogelea ambapo alijichanganya pamoja na na abiria wengine walionusurika na kuokolewa na vyombo vya uokozi. 

Wakati huo huo, Wapiga mbizi wa Vikosi vya Ulinzi na usalama leo wamefanikiwa kuzipata maiti nyingine za watu watano 
akiwemo mwanamke mmoja na wanaume wanne.

Katika upekuzi wa maiti hizo, Makachero wa Polisi walibaini kitambulisho cha kupigia kura kutoka kwa moja ya mwili
wa marehemu kitambulisho hicho  kilikuwa na jina la Philip John Busiya aliyezaliwa mwaka 1977 katika kijiji cha
Mapilinga kilichopo katika Kata ya Igokelo wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.  Kwa msaada wa Fullshangwe blog