Na Juma Mohammed,MAELEZO
Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein
ameagiza ndani ya wiki moja kuandaliwe utaratibu wa ununuzi wa meli ya abiria
na mizingo yenye uwezo wa kubeba abiria 1000.
Taarifa ya
Ikulu iliyotolewa jioni ya Julai 27 mwaka huu ilisema kwamba Rais Shein
ameiagiza Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo
kuanza mchakato huo.
Meli
inayotakiwa kununuliwa mbali ya kuwa na uwezo wa kubeba abiria 1000 kwa wakati
mmoja,pia iwe na uwezo wa kuchukua mizigo yenye uzito wa tani 100.
Katika
mazungumzo yake na Bodi ya Shirika la meli Zanzibar Rais Dk. Shein
aliwahakikishia wajumbe wa Bodi hiyo kuwa Serikali imedhamiria kununua meli ya
uhakika ili kurahisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Zanzibar.
Mbali
ya Bodi ya Shirika la Meli, katika kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi
wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na Wizara ya Nchi Afisi ya
Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo.
Agizo
la Rais Shein limeitaka Wizara yenye dhamana ya fedha kufanya kila wawezalo
kuhakikisha wanapata fedha kutoka vianzio vya ndani au nje ya nchi ama kutokana
na taasisi zinazohusiana na mambo ya fedha kununua meli hiyo.
Rais
Dk. Shein ameagiza pia katika kipindi kisichozidi miezi miwili
ujumbe wa Serikali uende katika makampuni yanayotengeneza meli nchini
Korea Kusini, China au Japan kwa ajili ya kuwasilisha fedha za utangulizi kwa
ajili ya utengenezaji wa meli hiyo.
Wakitoa
maelezo kwa Rais, Viongozi wa Shirika la Meli Zanzibar walisema kuwa meli
mpya yenye ukubwa inayotakiwa na Serikali huchukua muda wa mwaka mmoja
kutengenezwa.
Kikao hicho
ambacho kilikuwa na lengo la kuangalia mwelekeo na Mipango ya Shirika la Meli
pia, kilijadili hali halisi ya meli za Shirika la Meli na baadae
kujadili masuala ya ununuzi wa meli mpya itokayowaondoshea usumbufu
wa usafiri wa baharini wananchi wanaosafiri kati ya Unguja, Pemba na Tanzania
Bara. Kwa hisani ya Fullshangwe blog
|