Dk Slaa pia alitoa tamko ambalo limepitishwa na Kikao cha Kamati Kuu
iliyokutana tangu juzi kuhusiana na mpango wa usalama wa Taifa kutaka kuwadhuru
viongozi wa CHADEMA, Dk. Slaa amesema hawaoni sababu ya kuhojiwa na Jeshi la
Polisi kwa kuwa wamewahi kuwapa taarifa nyingi za vitisho dhidi yao na hakuna
hata moja imefanyiwa kazi.
“Hatuwezi kwenda Polisi kwa sababu tumekuwa tukipeleka mambo
mengi ya vitisho lakini hayafanyiwi kazi…na hili tulisha waambia hatuendi kwao
labda watukamate,” alisema Dk. Slaa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema yeye mwenyewe licha ya kuwasilisha madai mbalimbali
aliwahi kutegeshewa vinasa sauti na kutoa taarifa polisi lakini tangu wachukue
vifaa hivyo hawajasema chochote hadi leo, jambo ambalo limewafanya waamini hata
wakienda huko hakuna chochote kitafanyika.
Dk. Slaa alisema leo asubuhi alipigiwa simu na mmoja wa
maofisa upelelezi kutoka Makao Makuu ya Polisi akiomba miadi ya kukutana naye,
jambo ambalo amesema hayupo tayari kuhojiwa na wanausalama hao wa raia labda
wamkamate.
Alisema tayari baadhi ya viongozi wa Serikali wameanza
kuipuuza malalamiko yao dhidi ya vitisho wakidai huenda viongozi wa CHADEMA
wanatafuta umaarufu wa kisiasa kwa kutoa taarifa hizo, kitendo ambacho amesema
umaarufu wao hautatokana na viongozi wa Serikali au CCM bali ni kwa kazi
wanazozifanya kwa wananchi.
Juzi Dk. Nchimbi alisema taarifa za kutishiwa maisha dhidi
ya viongozi wa CHADEMA ni nzito hivyo haziwezi kupokelewa kirahisi Jeshi la
Polisi linaanza kazi ya kuwahoji wahusika ili kulifanyia kazi jambo hilo.
Alisema suala la usalama wa raia si hiyari bali ni la lazima hivyo hata kama
wahusika hawataki lazima taratibu zifanywe kuhakikisha usalama kwa wahusika.
|