AFYA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, Dk Steven Ulimboka imeanza kuimarika ingawa bado amelazwa katika
Chumba cha Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
Dk Ulimboka alipelekwa Afrika Kusini Juni 30, mwaka huu baada ya jopo la madaktari
lililokuwa likimtibu, likiongozwa na Profesa Joseph Kahamba kutoa taarifa za
kubadilika ghafla kwa afya yake na kupendekeza apelekwa nje ya nchi kwa ajili
ya vipimo na matibabu zaidi.
Jana, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage alisema taarifa
walizokuwa nazo zinasema: “Afya mwenyekiti wetu imeanza kuimarikia, lakini bado
yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi kwani alikuwa naumwa sana.”
Katika hatua nyingine, Dk Chitage alisema madaktari na wananchi wa kawaida
wanaendelea kutoa mchango wa awamu ya pili unaolenga kukusanya Dola za Marekani
30,000 kwa ajili ya kulipia gharama za matibabu za Dk Ulimboka.
“Sijapata kiwango sahihi kilichokusanywa hadi sasa, lakini michango inaendelea
vizuri. Madaktari na wananchi wanaendelea kukusanya na tunawashukuru,” alisema
Dk Chitage.
Madaktari na ndugu wa Dk Ulimboka kwa pamoja, walikataa ofa iliyokuwa itolewe
na Serikali ya kulipia gharama za matibabu za mgonjwa huyo wakiishutumu
kuhusika na tukio la kutekwa, kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Pande kwa
mwenyekiti huyo wa jumuiya ya madaktari.
Madaktari pia wamepinga tume ya polisi iliyoundwa na Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Suleman Kova wakitaka
kuundwa kwa tume huru kuchunguza tukio hilo.
Hilo ni miongoni mwa madai matano ya madaktari yaliyomo katika tamko la pamoja
baina yao na viongozi wa dini na wanaharakati.
Madai mengine ni pamoja na Serikali kurejea katika meza ya majadiliano na
madaktari, kufuta kesi iliyofungua mahakamani dhidi ya madaktari hao,
kuwarejesha kazini waliofukuzwa na Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi hao
kujadili chanzo cha mgogoro huo.
|