BABA wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, mzee
Steven Mwaitenda leo amesikitishwa mpaka kufikia kumwaga machozi mbele ya kadamnasi kwa uchungu alipoenda kumwona mwanaye aliyelazwa kutokana na mkasa wa kutekwa nyara na kujeruhiwa vibaya mwanae
Hali hiyo ilitokea jana jioni katika Taasisi ya Tiba
ya Mifupa Muhimbili (MOI), ambapo wanaharakati kutoka taasisi na asasi mbalimbali
za utetezi wa haki za binadamu walifika kwa lengo la kumpa pole Dk. Ulimboka
kufuatia kitendo kilichomfika.
Mzee Mwaitenda alijikuta akibubujikwa na machozi na
kushindwa kuendelea kuzungumza alipokuwa akitoa shukrani kwa wanaharakati hao,
kwa niaba ya mwanaye ambaye wanaharakati hao walishindwa kumuona wote kutokana
na hali yake ilivyo sasa.
“Niseme wazi nimefarijika sana kwa ujio wenu kumwona mwanangu dhidi ya
mambo ya kikatili aliyofanyiwa akitetea haki za wengine…,” alisema mzee
Mwaitenda kabla ya kushindwa kuendelea na kuangua kilio mbele ya wanaharakati.
Baada ya tukio hilo
baadhi ya wanaharakati walimshika wakishirikiana na wanafamilia ya mzee
Mwaitenda na kumbebeleza kisha kumtoa mbele ya mkusanyiko huo wa wanaharakati
na kumrudisha wodini huku wakimfariji.
Wakizungumza mara baada ya tukio hilo wanaharakati wameelezea kusikitishwa na
vitendo vinavyoendelea MOI eneo ambalo amelazwa kiongozi huyo wa madaktari
ambavyo vimeendelea kutishia usalama wa Dk. Ulimboka.
Akifafanua zaidi mwakilishi wa wanaharakati hao,
Markos Albania alisema taarifa walizozipata usiku wa juzi kuna wagonjwa ‘feki’
ambao walijitokeza MOI huku wakitaka kulazwa wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU)
alipolazwa Dk. Ulimboka lakini baadaye waligoma kuingizwa wodini.
“Wapo wagonjwa ambao waliletwa na kutaka kupelekwa
ICU moja kwa moja…kuna watu wanakuja usiku wa manane wakitaka kumtembelea Dk.
Ulimboka…matendo yanayoendelea kutokea ukilinganisha na kauli za Serikali
zilizotolewa bungeni yanatishia usalama na uhai wa mgonjwa,” alisema Albania.
Aidha amesema kitendo cha vyombo vya usalama
kuendelea kumuhoji Dk. Ulimboka akiwa hoi hospitalini si vya kiungwana kwani
tayari muhusika amewataja hadi kwa majina watu ambao anawashuku lakini hadi
sasa hakuna aliyechukuliwa hatua yoyote.
Pamoja na hayo wanaharakati hao wameitaka Serikali
kuunda tume huru mchanganyiko na raia ambayo itachunguza kiundani suala hilo, kwani hawana imani na Jeshi la Polisi ambalo limedai
kuunda timu ambayo inachunguza kwa kina suala hilo.
Dk. Ulimboka ambaye ni kiongozi wa madaktari ambao
wanaendelea na mgomo wan chi nzima kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yao alitekwa juzi na watu
wasiojulikana na kupigwa na kuteswa kikatili kabla ya kutelekezwa katika msitu
wa Mabwepande.