HOSPITALI ya Amana Jijini Dar es Salaam imeingia katika kashfa nyingine baada ya mwanamke mmoja kudaiwa kujifungua akiwa amesimama na kusababisha kichanga kilichozaliwa kuanguka sakafuni.
Tukio hilo limetokea Jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki iliyopita, majira ya saa 11: 30 jioni baada ya mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Kuruthum Abdallah (30) mkazi wa Majohe kufikishwa hospitalini hapo kwa ajili ya kupata huduma ya kujifungua.
Akiongea akiwa nyumbani kwake, Kuruthum alisema kabla ya kutokea tukio hilo, alilazimishwa kusimama na muuguzi wa zamu wa siku hiyo kwa ajili ya kutoa maelezo licha ya kuonekana yupo katika hatua ya mwisho ya kujifungua.
Alisema mara baada ya kufika Hospitali hapo akisindikizwa na mumewe Jabir Yahya (38) pamoja na jamaa zake, alipelekwa katika wodi wazazi namba sita maalum kwa ajili ya kujifungua.
Licha ya kuonekana kuwa na dalili zote za mwisho ili aweze kujifungua, muuguzi aliyekuwa zamu siku hiyo alimtaka kwenda kubadilisha nguo zake na kisha amfuate hadi kwenye meza yake ili atoe maelezo yake.
Alieleza alipoelezwa hayo, alimjibu asingeweza kufanya hivyo kwa sababu ana kila dalili ya kujifungua kwa wakati huo na kumuomba ampeleke kwenye chumba cha kujifungulia (leba).
Hata hivyo, muuguzi huyo alionekana kuwa mkali na kumtaka afanye kama alivyomueleza kwani wakati kudeka umekwisha kwa kuwa hata huo ujauzito wakati anaupata hakuwepo.
Kuruthum alisema baada ya kujibiwa hayo, alimua kumfuata muuguzi huyo hadi katika meza yake, lakini kipindi hicho uchungu uliongezeka kiasi cha kutoweza kusimama vizuri.
"Nilikwenda hadi katika meza yake na kuanza kuniuliza maswali, kwa kweli nilichoweza kujibu ni maswali machache tu kwani uchungu ulizidi, nilijaribu kumwambia tena hakunisikiliza," alisema Kuruthum.
Kutokana na kukabiliwa na maumivu makali ya uchungu, alijaribu kumshika muuguzi hyo ili asikilize anachomueleza, hata hivyo hakumsikiliza na badala yake alikuwa mkali.
"Aliniambia usiniguse unichafulie nguo, lakini nilijitahidi kusimama huku nikijaribu kujibu maswali yake japokuwa mengine yalinipita kutokana na uchungu niliokuwa nao," alisema.
Alisema wakati anahangaika kujibu maswali, ghafla alishtukia mtoto akitoka kwa kasi na kuangukia sakafuni.
"Nilishtukioa mtoto akitoka na kuangukia sakafuni na kisha kuserereka hadi chini ya meza, tukio lilinishtua sana na hata watu waliokaa mlangoni walipiga kelele ya hofu," alisema mama huyo.
Baada ya kuona hivyo muuguzi huyo alifunga haraka mlango, kisha alimuokota mtoto huyo ambaye kipindi hicho alikuwa akilia na kumpeleka kwenye chumba cha wazazi kwa kumsafisha.
Hata hivyo mume wake Yahya alisema tukio hilo alishuhudia kwa macho yake na lilimuogopesha sana kiasi cha kutokuwa na matumaini ya kumpata kichanga akiwa hai.
Hata hivyo anamshukuru Mungu kwa kufanya miujiza ya kumuokoa mwanawe huyo ambaye amempa jina la Arafa lenye maana ya shukurani.
"Mungu ni mkubwa kwani sikuamini kabisa nilichokiona pale, lakini yote namtupia Mungu kutokana na uzembe uliosababisha maisha ya mwanangu kuwa hatarini," alisema Yahya.
Akizungumzia tukio hilo, Daktari Kiongozi wa Hispo\itali hiyo Shauri Mwaluka alisema kimsingi hawajapata malalamiko yoyote kutoka kwa wazazi wa mtoto huyo, hivyo aliwataka wazazi hao kwenda ofisini kwake kutoa malalamiko yao rasmi ili yafanyiwe kazi.