Kikosi cha Bongo Movies
Kikosi cha Twiga Stars
Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake
(Twiga Stars) itacheza mechi ya kirafiki na timu ya wasanii wa filamu ya Bongo
Movie itakayofanyika Jumamosi (Aprili 14 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Lengo la mechi hiyo ya
maonesho (exhibition) ni kuichangia Twiga Stars ambayo hivi sasa iko kwenye
mashindano ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) ambayo fainali zake
zitafanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Pia asilimia mbili ya mapato
yatakayopatikana kwenye mechi ya Twiga Stars na Bongo Movie yatakwenda kwenye
familia ya mwigizaji nguli wa filamu Tanzania, Stephen Kanumba aliyefariki dunia
Aprili 7 mwaka huu.
Kiingilio katika mechi hiyo
kitakuwa sh. 10,000 kwa VIP A, sh. 5,000 kwa VIP C na B na sh. 2,000 kwa viti
vya rangi ya chungwa, kijani na bluu. Mechi itaanza saa 10 kamili
jioni.
Twiga Stars itacheza mechi ya kwanza ya
mchujo dhidi ya Ethiopia jijini Addis Ababa. Mechi hiyo itachezwa Mei 26 mwaka
huu na wiki mbili baadaye timu hizo zitarudiana jijini Dar es Salaam. Twiga
Stars ilifuzu raundi hiyo baada ya kuitoa Namibia kwa jumla ya mabao
7-2.