Friday, April 13, 2012

UBALOZI WA TANZANIA INDIA WASHEREKEA USHINDI WAO

Na fullshangw blog


Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania [New Delhi] nchini India tarehe 8 mwezi huu [Aprili 2012] ulifanya hafla kubwa kusherehea ushindi na kuipongeza Timu ya Mpira wa Miguu ya Ubalozi kwa kunyakua Ubingwa wa Mashindano ya  "United Cup 2012" ambayo huzishirikisha Timu za Balozi mbali mbali zilizoko nchini India [ Inter Embassies] . 

Timu ya  ya Ubalozi wa Tanzania iliibuka kidedea  kwa kuifunga Timu ngumu ya Ubalozi wa Botswana magoli mawili.  Mashindano haya  yalianza rasmi tarehe 29 Machi na kufikia kilele [fainali] tarehe  1 Aprili 2012.
Timu ya Ubalozi  ilijumuisha Familia za Maafisa wa Ubalozi na Wanafunzi wa Tanzania wanosoma katika Jimbo la Delhi pamoja na Majimbo mengine ya jirani.  

Vile  vile, Timu ya Ubalozi ilishinda mechi zote za awali kabla ya kufanikiwa kuingia fainali.  Timu ya Ubalozi wa Botswana ilichukua nafasi ya pili na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Timu ya Ubalozi wa Saudi Arabia.

Balozi nyingine zilizoshiriki katika Mashindano haya ni Denmark, China, Spain, France, Egypt, Saudi Arabia, Indonesia, Netherlands na Israel,  United Nations na Timu ya “Touch of Hope Foundation” na wenyeji  India.
Mashindano haya huandaliwa  "New Delhi United Football Club" kwa kushirikiana na Wadau wengine  kwa madhumuni ya kuimarisha urafiki, Ushirikiano,  upendo na kujenga afya za  washiriki.