Tuesday, April 10, 2012

SIMBA KUCHAPANA NA TP MAZEMBE

Na Mwandishi Wetu
 
 KATIKA kuhakikisha Simba inazidi kuimarika kwa michuano ya Kombe la
Shirikisho Afrika, mfanyabiashara maarufu na mwanamichezo Azim Dewji
anakusudia kuileta nchini timu ya soka ya TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa ajili ya kuipa makali Simba kabla ya
wawakilishi hao wa Tanzania hawajaivaa Al Ahly Shandy ya Sudan.
Dewji aliyeifadhili Simba kwa miaka mingi, alisema jana Dar es Salaam
kuwa ziara inaratibiwa na kampuni yake ya Simba Trailers na kwamba
ameshazungumza na kuafikiana na Rais wa Mazembe, bilionea Moise
Katumbi Chapwe na pia uongozi wa Simba.
 “Pamoja na kuwazawadia pesa wachezaji wa Simba, nimeona nitoe mchango
zaidi kwa kuwaletea mechi ya kujipima nguvu na timu bora ya Mazembe ya
Kongo,” alisema Dewji aliyetoa sh milioni 15 kwa Simba baada ya kuitoa
ES Setif ya Algeria.
Kwa mujibu wa Dewji, mchezo baina ya Mazembe na Simba unatarajiwa
kufanyika Aprili 22 mwaka huu jijini Dar es Salaam, ikiwa ni wiki moja
kabla ya `Wekundu wa Msimbazi’ kuumana na Al Ahly.
Alisisitiza kuwa, Mazembe itakuwa kipimo sahihi kwa Simba kutokana na
kuwa na kikosi chenye hadhi ya juu.
Mazembe iiliyotwaa ubingwa wa Afrika mara nne, ikiwa pamoja na mwaka
2009 na 2010 kabla ya kuondolewa mashindanoni mwaka jana kutokana na
dosari katika usajili wake, inajivunia utajiri mkubwa wa fedha na
vipaji vya mastaa kama Muteba Kidiaba, Tresor Mputu, Given Singuluma,
Stoppila Sunzu, Rainford Kalaba, Patrick Ochan na washambuliaji raia
wa Tanzania, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu.
Licha ya kutikisa katika Ligi ya Mabingwa Afrika katika miaka ya hivi
karibuni, Mazembe pia ilitamba katika Klabu Bingwa wa Dunia mwaka 2010
huko Japan ambako ilifika fainali, hatua ambayo haikuwahi kufikiwa na
klabu yoyote ya Afrika katika michuano hiyo.
“Kupambana na kikosi bora kwa Afrika wakati kama huu itakuwa bahati
kubwa kwa Simba, tuombe Mungu mambo yote yaende vizuri ili wawakilishi
wetu wanoe makali ya kuitikisa zaidi Afrika katika Kombe la
Shirikisho,” alisema.
Wakati Simba imetinga raundi ya tatu kwa kuing’oa Setif kwa jumla ya
mabao 4-3, Al Ahly Shandy imeitupa nje ya michuano ya mwaka huu
Ferroviario ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 3-0.
Mshindi baina ya Simba na Al Ahly Shandy atatinga hatua ya Nane Bora
ambayo timu nne kuchuana katika kila kundi kusaka tiketi ya nusu
fainali.
Nayo Mazembe, licha ya kujipima na Simba kwao itakuwa fursa ya
kuongeza makali ya kushiriki katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kwani
nayo imesonga mbele baada ya mwishoni mwa wiki kuifumua Power Dynamos
ya Zimbabwe kwa 6-0. Timu hizo zilifungana 1-1 katika mchezo wa kwanza
huko Harare, Zimbabwe.