Aliyekuwa kocha wa Yanga Sam Timbe.
UONGOZI wa mabingwa watetezi wa
ligi kuu soka Tanzania Bara, Yanga uko mbioni kumrejesha kukinoa kikosi hicho
aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mganda Sam Timbe.
Timbe ambaye aliiwezesha Yanga
kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2010/2011 na kombe la Kagame, mkataba wake
ulivunjwa msimu uliopita kwa madai ya kushindwa kuiletea mafanikio timu hiyo na
nafasi yake kujazwa na Mserbia Kostadin Papic.
Habari za uhakika kutoka ndani
ya klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Jangwani na Twiga zinaeleza kuwa
Timbe atarejea kukinoa kikosi hicho wakati wowote kuanzia sasa akirithi mikoba
ya Papic.
Imeelezwa kuwa mkataba wa Papic
umebakiza siku chache kumalizika na uongozi hauna mpango wa kumuongeza mkataba
mkataba mpya,kutokana kutomuhitaji tena.
Mmoja ya viongozi wa Yanga
ambaye hakupenda kutajwa jina lake aliliambia gazeti hili kwamba hawana mpango
tena na Papic kutokana na kutokuwa na jipya ndani ya klabu hiyo hivyo
wanaendelea na mikakati ya kumrejesha Timbe.
“Mimi nashangaa huyu kocha
anazungumza na vyombo vya habari kuwa hajalipwa miezi mitatu, huo ni uzushi
ambao hauna maana yoyote...ninachoona ni kutaka kuudanganya umma ili adanganye
kuwa kaondoka kwa kutolipwa wakati mkataba wake ulishakwisha,”Aliongeza.
Baadhi ya vyombo vya habari leo
viliripoti kocha hutyo kutoambatana na timu Kanda ya Ziwa kutokana na kuugua
Tumbo na mafua huku pia ikidaiwa kocha huyo hajalipwa mshahara wake kwa miezi mitatu
hali inayomuweka katika mazingira magumu ya ufundishaji wake.
Hata hivyo ofisa habari wa Yanga
Louis Sendeu alisema jana kuwa taarifa za Papic kudai mshahara hazina ukweli
wowote na kukiri kuwa kocha huyo ni mgonjwa ndio maana hajaambatana na timu
katika safari hiyo , lakini kama hali yake itatengemaa huenda akaungana na timu
hiyo leo.
Alisema kikosi cha timu hiyo
kinanatarajiwa kuondoka Kahama leo kwenda Mwanza tayari kwa mechi yao ya Ligi
Kuu soka Tanzania Bara ambapo jumapili kitashuka kwenye dimba la CCM Kirumba,
jijini humo kukwaana na wenyeji Toto African.