Wednesday, April 11, 2012

KINADADA wanaoishi maeneo ya Buguruni mtaa wa Madenge jijini Dar es Salaam wamelalamika kunyanyaswa na kunyimwa uhuru wa kuishi baada ya kikundi kinachojitambulisha kama ulinzi shirikishi kuwavamia na kuwafukuza wakihisi kuwa wanafanya ukahaba.

Wakizungumza na Blog hii kinadada hao walikanusha kufanya biashara hiyo na kusema kuwa wanahisiwa hivyo kwakuwa vyumba vyao vinamilango miwili na  waliambiwa wazibe na wakaziba ila bado wananyimwa uhuru wa kuishi.

Blog hii ilimtafuta mlalamikiwa ambaye ni kiongozi wa kikundi hicho cha ulinzi shirikishi aliyejitambulisha kwa jina la Khalid Juma maarufu kama Sheikh Ndevu, na kusema kuwa wao hawamnyimi mtu haki ya kuishi na kuwa, kinadada hao wanaruhusiwa kurudi kwenye nyumba zao na kuendelea kuishi kwakuwa tayari milango yote ya ziada imeshafungwa.

Aidha kinadadas hao wamesema kuwa wanataka kuishi kwa uhuru kwani mpaka sasa hakuna mgeni yeyote anayeruhusiwa kuingia kwao hata kama ni ndugu yao.

Pia mwandishi wa blog hii alifanikiwa kuongea na Diwani wa kata hiyo ya Buguruni na kusema kuwa, wananchi wake wanatakiwa kuishi kwa amani pasipo ya kuwa na kusumbuliwa kwani hatambui uwepo wowote wa kikundi cha ulinzi shirikishi katika kata yake.

Kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi wa ilala alipotafutwa kuzungumzia sakata hili hakupatikana hata kwa kupitia simu yake ya mkononi.

Tutaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusiana na sakata hili.