Akijibu swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent
Nyerere (CHADEMA) aliyehoji Serikali ina mpango gani wa kusitisha kutoa
Mikataba kwa wastaafu ili wahitimu wanaotoka vyuoni wapate ajira,
waijenge nchi yao Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma, Celina Kombani amesema Serikali itaendelea na utaratibu wa
kuwaajiri wastaafu katika kada za uhandisi, ualimu, uganga na wahadhiri wa vyuo vikuu mpaka hapo soko la ajira litakapojitosheleza.
“Hilo linatokana na utaalamu walionao ambao ni vigumu kuziba nafasi zao kwa kipindi cha haraka.” alisema Kombani.
Waziri
alisema ni kweli kuwa wako wataalamu wengi wanaohitimu vyuo vikuu hapa
nchini ambao wanahitaji kuingia katika soko la ajira, lakini hupatiwa
ajira kulingana na uwezo na bajeti ya Serikali.
Kwa
sasa Serikali inawapa mikataba ya muda mfupi wataalamu wastaafu wa kada
hizo ambao sio rahisi kuwapata katika soko la ajira, sanjari na
kuwaajiri wahitimu wa vyuo mbalimbali. Waraka wa Rais namba 1 wa mwaka
1998 unatamka kwamba endapo utaalamu wa mtumishi unahitajika sana,
Serikali inawajibika kumwomba mtumishi kuendelea kufanya kazi na siyo
mstaafu mwenyewe kuomba.
Katika swali la nyongeza la Nyerere kuwa
Wakuu wa mikoa wengi ni wastaafu lakini wameajiriwa serikalini, Kombani
alisema, “wakuu wa mikoa si watumishi wa umma na wapo katika utumishi
wa kisiasa kama walivyo wabunge”.
Katika swali la nyongeza,
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR Mageuzi) aliyetaka kufahamu
kwa nini Serikali haijawaajiri walimu waliomaliza Shahada ya Ualimu
katika Saikolojia katika Chuo cha Ualimu Dar es Salaam (DUCE) wakati
ilipoajiri walimu wengine, Kombani alijibu, “Kweli mwanzoni tulipoajiri
wao hatukuwaajiri lakini sasa Serikali inafanya utaratibu ili iwapangie
kazi wahitimu hao”
No comments:
Post a Comment