Saturday, April 13, 2013

EMBU TUJIKUMBUSHE KUHUSU SOKOINE NA NUKUU ZAKE

Marhemu ndugu Edward Moringe Sokoine alizaliwa tarehe 01.08.1938.

Alifariki tarehe 12 Aprili 1984 katika ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Wami-Dakawa wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, wakati akitoka Bungeni Dodoma kurejea jijini Dar es Salaam. Gari lake liligonga uso kwa uso na gari jingine lililokuwa likitokea Morogoro Mjini. Katika ajali hiyo, Sokoine pekee ndiye aliyepoteza maisha!

Sokoine aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa  Tanzania aliyeiongoza katika kipindi kigumu sana ya kiuchumi na kuwa mwiba mkali kwa wahujumu uchumi.  Hizi ni baadhi ya nukuu za kauli zake:
“Ole wake kiongozi mzembe na asiye na nidhamu nitakayemkuta: Kiongozi wa siasa hana usalama wa aina yoyote. Usalama wake ni kudra ya Mungu na Wananchi peke yake. Viongozi wazembe na wabadhirifu wahesabu siku zao. Labda tusiwajue. Hawa hatuna sababu ya kuwapa imani, kuwa tutawalinda kama vitendo vyao viovu” - 26 Machi 1983
“Vijana leo wengi wana mali zaidi kuliko wazee waliofanya kazi miaka thelathini hadi arobaini. Lakini wanaitaka Serikali ndiyo iwaulize mali hiyo wameipata wapi. Hivi kwa nini mzazi asimuulize mwanae, 'mali hii umeipata wapi?” - 23 Oktoba 1983
“Wajibu wa kila Mtanzania, kila familia na kila anayekula ni kujilisha mwenyewe. Si wajibu wa Taifa kumlisha mtu. Unaweza ukasaidiwa unapopatikana na janga. Lakini kama hakuna janga ni wajibu wa kila mtu aweze kujitosheleza kwa chakula na atoe ziada kwa Taifa” - 4 Oktoba 1983
“Serikali inasimamia bei, lakini Serikali yetu itakwenda mpaka itasimamia bei ya mhogo, dagaa na bei ya kila kitu? Haiwezekani, vitu vingine ni lazima vizalishwe kwa wingi ili bei yenyewe iweze kujirekebisha” - 24 Septemba 1983
“Juu ya suala hili la mapato kutolingana na matumizi ni kwamba tungependa kupunguza uongezaji wa wataalam wasiohitajika katika Serikali na katika mashirika ya umma mpaka hapo hali yetu ya uchumi itakapokuwa katika hali nzuri” - 23 Oktoba 1982
“Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi yawe ni chombo cha kulinda haki na maslahi ya walio wengi. Na kamwe hayaruhusiwi kuwa ni chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao na kusahau maslahi ya walio wengi” - 1Februari 1977.
Picture
Serikali ilijenga mnara kwenye eneo la ajali ya Sokoine kwa lengo la kumkumbuka kiboko huyo wa wahujumu uchumi. Februari 2013, Dustan Shekidele alitembelea eneo la kumbukumbu ya ajali, ambapo alimkuta mlinzi wa eneo hilo Bw Mpanda Chalo aliyesema kwamba Serikali ina mpango wa kujenga shule ya sekondari nyuma ya mnara huo kwa lengo la kumuezi kiongozi mwadilifu, Edward Moringe Sokoine.

No comments:

Post a Comment