Saturday, December 22, 2012

CHUO CHA SAYANSI NA TIBA MUHIMBILI KUJENGA HOSIPITALI NA CHUO KIBAMBA

CHUO kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas) kinatarajia kujenga hospitali na chuo katika eneo la Mloganzila Kibamba, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Hospitali hiyo itakuwa ya kisasa inayowiana na ile ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambapo kukamilika kwake itakuwa na vitanda 600.
Mkurugunzi wa Mipango na Maendeleo ya mradi mpya wa ujenzi tawi la Muhas, Appolinary Kamuhabwa alisema hayo juzi wakati Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge alipotembelea eneo hilo.
Alisema ujenzi huo wa hospitali ambao utatekelezwa kwa pamoja na ujenzi wa chuo cha afya kama kile Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas), utagharimu Sh bilioni 600.
“Mradi huu ni wa awamu mbili, ambapo kwa kuanza tunaanza kujenga hospitali na ujenzi huu utaanza Februari mwakani na kukamilika ndani ya miezi 24 ambapo  utagharimu Sh bilioni 120,”alisema Kamuhabwa
“Awamu ya pili ni ujenzi chuo ambapo lengo la ujenzi huo ni kupanua Campas yetu ya Muhimbili, na mpaka kukamilika kwa miradi yote miwili Sh bilioni 600 zinatarajia kutumika ili kukamilisha mradi huo pamoja na vifaa vya hospitali,”aliongeza
Vile vile Kamuhabwa alimuomba naibu waziri wa Maji Dr Mahenge kuwapatia maji eneo hilo pindi ujenzi huo utakapo anza kutokana na eneo hilo kuwa na uhaba wa maji kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Naibu waziri wa maji alisema  kwa sasa wameagiza kuwepo kwa mikakati ya kuwepo kwa maji ya muda mfupi kwa ajili ya ujenzi huo kabla ya kufungwa mabomba katika eneo hilo.
 
Naye Mkurugenzi wa ufundi kutoka Dawasa Mhandisi Boniface Kassiga alisema kuwa wizara itahakikisha kuwa kabla ya kuanza kwa ujenzi huo maji  ya muda mfupi yatapatikana kabla.
Eneo la Mloganzira lipo karibu na eneo la Kwemba Kibamba ambapo ni katikati Manispaa ya Kinondoni na Wilaya ya Kisarawe.

No comments:

Post a Comment