Saturday, November 10, 2012

YANGA KUMALIZA LIGI LEO KWENYE UWANJA WA MKWAWANI TANGA

Na Mahmoud Zubeiry
MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unakamilishwa leo kwa mechi moja kali kupigwa kwenye Uwanja wa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kati ya wenyeji Coastal Union na vinara wa ligi hiyo, Yanga SC.
Yanga imepania kushinda mechi hiyo ili kujiweka katika mazingira mazuri katika msimamo wa Ligi Kuu, ambayo mzunguko wake wa pili utarejea Januari mwakani.
Wchezaji wa Yanga inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts wamepania kuvunja rekodi ya Coastal Union kutofungwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani, Mkwakwani, Tanga katika mechi hiyo.
Nahodha Msaidizi wa Yanga, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ alisema kwamba wanataka kustawisha uongozi wao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kuwafunga Coastal Jumamosi.
Alisema wanajua Coastal ni timu nzuri na wanatarajiwa upinzani katika mechi hiyo, ila ameonya Yanga ya sasa ni tishio na wachezaji wako vizuri ‘ile mbaya’.
Lakini pia habari za ndani kutoka Yanga zinasema kwamba tayari wachezaji wameahidiwa donge nono iwapo watashinda mechi hiyo.
Wachezaji hao, walizawadiwa Sh. Milioni 15 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC mwishoni mwa wiki katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 26 na ikishinda dhidi ya Coastal itakwenda kupumzika kwa raha sana. 
Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal, Nassor Bin Slum amesema Yanga watake wasitake watafungwa Mkwakwani leo. Msimu uliopita, Yanga waliifunga Coastal mechi zote, kwanza 5-0 Dar es Salaam na 1-0 Tanga.
Lakini Coastal ya mwaka huu ni nyingine kabisa, kwani imesajili wachezaji wazuri na wazoefu. Nsa Job hatakuwapo kwa sababu anaumwa goti, lakini yupo mkali mwingine wa mabao katika timu hiyo, Daniel Lyanga.
Burudani zaidi inatarajiwa kuwa katika safu ya kiungo, Coastal kuna Razack Khalfan na Jerry Santos na Yanga wapo Athumani Iddi ‘Chuji’ na Haruna Niyonzima. Yanga wameshinda mechi mbili za ugenini kati ya tano, wametoa sare moja, wamefungwa mbili pia.
Katika mechi za jana, bao pekee la Mussa Said Kimbu dakika ya 73, leo liliizamisha Simba SC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kimbu alifunga bao hilo akiunganisha krosi ya Mganda, Mohamed Jingo tena akipitisha mpira katikati ya msitu wa mabeki wa Simba na kipa wao, Wilbert Mweta.
Katika michezo mingine ya ligi hiyo, Azam ilifungwa 2-1 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, African Lyon ikafungwa 3-1 na Mtibwa Sugar, Kagera Sugar ikatoka sare ya bila kufungana na Polisi Morogoro, JKT Oljoro ikafungwa 3-1 na Ruvu Shooting na Prisons ikatoka sare ya 1-1 na JKT Ruvu.

No comments:

Post a Comment