Moja ya kipeperushi kilichotengenezwa kwa ajili ya kumng'oa Kikwete |
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinaanza mkutano wake mkuu leo mjini Dodoma, vita ya makundi ya urais 2015, imeshika kasi kwa makada wake kutajana hadharani kuhusika kusambaza vipeperushi vya kutaka kumhujumu na kumng’oa Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Makundi yaliyoingia katika mzozo huo, moja linadaiwa kuwa la wafuasi wa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na lingine la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, kila moja likitaka kuwa karibu na Rais Kikwete.
Hatua ya makada wa makundi hayo ya CCM kutajana na kushutumiana hadharani kutaka kumhujumu mwenyekiti wao wa taifa, imekuja siku chache baada ya hivi karibuni gazeti hili kufichua uasi huo, ili wajumbe wa mkutano mkuu wampigie kura za maruhani kuonyesha kutokuwa na imani nae.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana mjini hapa, mjumbe wa Mkutano Mkuu, Husein Bashe alimtaja hadharani Waziri Membe kwamba anahusika kusambaza vipeperushi vya kumhujumu Rais Kikwete.
Bashe aliamua kumlipua Membe baada ya yeye pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, kutajwa kuhusika na uasi huo.
Wengine waliotajwa kuhusika na vipeperushi hivyo ni Beno Malisa, na Fred Lowassa kuwa ndio wanahusika na njama hizo.
Vipeperushi hivyo vimeandikwa kuwaomba wanachama wa CCM kumpigia kura ya hapana Kikwete kwa madai kwamba chama kinayumba, hivyo apunguziwe mzigo ili abaki na urais tu.
No comments:
Post a Comment