Thursday, November 1, 2012

WAZIRI ASEMA DNA ITABAINI PEMBE ZA NDOVU ZILIZOKAMATWA HONG KONG

Nukuu ya gazeti la NIPASHE

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema shehena na makontena mawili ya meno ya tembo yaliyokamatwa Hong Kong, yatachunguzwa kwa kutumia vinasaba (DNA) ili kubaini kama asili yake ni Tanzania.

Aidha, amesema maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wale waliokuwa zamu siku shehena hiyo ikipitishwa bandarini Dar es Salaam kwenda Hong Kong, wanachunguzwa ili kubaini ukweli.

Alisema hayo wakati akifanya majumuisho ya hoja za wabunge waliokuwa wakijadili maazimio mawili ya Bunge kuhusu marekebisho ya mpaka na upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe na lile la kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane, “Hatuna uhakika bado kama meno yaliyokamatwa huko Hong Kong yana asili ya Tanzania au yalikuwa yakipitishwa nchini mwetu…tunafanya mazungumzo na balozi wetu kule China kuhusu suala hilo,” alisema.

Alisema taarifa ambazo zimekwishapatikana zinaonyesha kwamba kontena moja linatokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kontena lingine bado halijaeleweka wazi kwamba linatokea Tanzania au la, na ndio maana uchunguzi utahusisha vipimo vya DNA ili kujua asili ya meno hayo.

Oktoba 16, mwaka huu, maofisa usalama wa Hong Kong waliyakamata makontena mawili yaliyokuwa yamesheheni meno ya tembo yenye thamani ya dola za Marekani milioni 3.4. Hata hivyo, kontena moja kati ya hayo lenye thamani ya dola za Marekani milioni 1.7 linadaiwa kuwa linatokea Tanzania. Kama hiyo haikutosha, shehena ya meno ya tembo ilikamatwa bandarini Dar es Salaam Jumapili iliyopita na hali ambayo inaonyesha kasi ya kuuwa kwa tembo ni kubwa.

Mapema katika mchango wake binafsi, mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa, alisema kuongeza mipaka ya hifadhi ni suala zuri lakini serikali inawajibu wa kulinda hifadhi hizo.

Alizungumzia tukio la hivi karibuni la kukamatwa kwa meno ya tembo huko Hong Kong na bandarini Dar es Salaam yanaashiria kwamba tembo waliopo kwenye hifadhi wanauawa, “Hii inaonyesha jinsi gani tembo wetu wanavyoteketea,” alisema na kuongeza, “sifurahishwi sana kuona tembo wetu wanakufa.”