Sheilla Sezzy, Mwanza
POLISI mkoani hapa wamefanikiwa kuipata simu ya upepo ‘radio call’
iliyokuwa ikitumiwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
marehemu Liberatus Barlow ambayo ilichukuliwa baada ya kuuawa kwa
kupigwa risasi usiku wa manane eneo la Minazi Mitatu Kitangiri.
Mbali na simu hiyo, jeshi hilo pia limefanikiwa kupata ufunguo wa gari
la marehemu Barlow ambaye aliuawa wakati akimsindikiza mwanamke mmoja
aliyeitwa Doroth Moses walipokuwa wakitoka kwenye kikao cha harusi ya
ndugu yake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lili Matola, alisema jana kwamba
vitu hivyo vilipatikana vikiwa vimefichwa katika shimo la majitaka
katika nyumba moja iliyopo maeneo ya Nyashanya.
Pia jeshi hilo limefanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wengine wawili
wanaodaiwa kuhusika katika mauaji hayo na Kamanda Matola alisema
wataunganishwa kizimbani na wengine watano Novemba 15, mwaka huu.
Alisema watuhumiwa hao wawili (majina tunayahifadhi kwa sasa), mmoja
wao akiwa ni ndugu wa mtuhumiwa namba moja katika mauaji hayo, ndio
waliotaja sehemu vilikokuwa vimefichwa vitu hivyo baada ya kuhojiwa.
“Baada ya kuonyesha vilipokuwa vimefichwa, ilibidi kumtaarifu mwenye
nyumba ambaye alitoa idhini ya kubomolewa kwa shimo hilo la majitaka na
mmoja wa watuhumiwa aliingia na kutoa ‘radio call’ pamoja na funguo za
gari la marehemu,” alisema Kamanda Matola.
Alisema kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa namba moja
alitoa maelekezo ya wapi pa kuficha vifaa hivyo. Kabla ya kuficha simu
hiyo, waliitenganisha na betri yake.
Kamanda Matola alisema katika msako waliofanya nyumbani kwa watuhumiwa
hao, pia walikuta sare za moja ya kampuni ya ulinzi pamoja na magwanda
ya mgambo.
Mbali na watu hao, Matola alisema polisi pia inamshikilia mtu mmoja
(jina tunalihifadhi) mkazi wa Nyakabungo akituhumiwa kufadhili kundi
hilo la majambazi.