KADA
maarufu na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Abdulrahman Kinana, amesema hausiki na usafirishaji wa meno ya tembo
nje ya nchi, ikiwa ni siku moja tu tangu gazeti moja la wiki, lichapishe
habari iliyomuelezea kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni iliyosafirisha
meno hayo.
Hata hivyo, kada huyo amekiri kuwa mmiliki wa Kampuni ya uwakala wa meli
ya Sharaf Shipping Agency, iliyohusika kusafirisha makontena yaliyokuwa
na nyara hizo za serikali, kabla ya kukamatwa nchini China yakiwa
safarini kupelekekwa Hong Kong.
Gazeti hilo lilimtaja Kinana kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo kwa
kuwa na hisa 7,500 kati ya 10,000 katika kampuni hiyo, huku hisa
nyingine 2,500 zikiwa zinamilikiwa na mshirika mwenzake, Rahma Hussein.
Thamani ya hisa hizo ni sh 1,000 kila moja.
Kinana alitoa ufafanuzi huo katika mahojiano maalum na Tanzania Daima.
“Nimeisoma habari hiyo na kwa bahati mbaya sioni anayenilaumu wala kitu
ninacholaumiwa nacho. Kwamba nina hisa katika kampuni ya wakala wa meli
ya Sharaf ni kweli.
“Lakini mimi sina nafasi yoyote ya kiutendaji na wala sishughuliki na
uendeshaji wa kampuni hiyo. Kwa kweli sikujua na wala sikuhusika kwa
namna yoyote ile na usafirishaji wa makontena hayo na mengine yoyote,”
alisema Kinana.
Alisema anachojua yeye ni kwamba, maofisa wa kampuni hiyo waliuliza na
kuambiwa kuwa shehena iliyokuwa katika makontena hayo ni plastiki
zilizotumika.
Alifafanua kuwa, wenye wajibu na mamlaka ya kukagua shehena zote
zinazosafirishwa nje ya nchi ni mamlaka za serikali na si kampuni ya
uwakala wa meli.
Alisisitiza kuwa, hana mamlaka kwa mujibu wa sheria kukagua mali
inayosafirishwa japokuwa anaweza kuuliza bidhaa iliyopo katika makontena
hayo.
“Ni dhahiri kabisa kwamba, habari hii imeandikwa na jina langu kutumika
katika malengo ambayo siyajui. Nahisi kama jina langu limetumika kama
pilipili katika kachumbari ili kunogesha habari.
“Kwa bahati mbaya pilipili imezidi katika kachumbari. Kama lengo
lilikuwa kupasha habari, basi umma umedanganywa,” alisema Kinana.
Kwa mujibu wa habari hiyo, sakata la kukamatwa kwa nyara hizo za
serikali liliibuliwa kwa mara ya kwanza na Mbunge wa Same Mashariki
(CCM), Anne Kilango Malecela, katika Bunge lililopita la bajeti.
Ilidaiwa kuwa, nyaraka hizo zilionyesha kuwa, kilichokuwa ndani ya
makontena hayo ni plastiki zilizodurufishwa na baada ya ukaguzi
kufanyika, iligundulika kuwa, kilichokuwemo ni pembe za ndovu.
Habari ya gazeti hilo hata hivyo, ilimnukuu ofisa mwandamizi wa Wizara
ya Viwanda na Biashara, akieleza wazi kuwa kazi ya kukagua kilichomo
kwenye kontena linalosafirishwa si ya wakala wa meli kwani, wenye
mamlaka na idhini ya kufanya hivyo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

No comments:
Post a Comment