JESHI la Polisi limewataja watuhumiwa 10, na bado linaendelea kuwatafuta
watuhumiwa wengine, ambao inadai walishiriki kumuua aliyekuwa Kamanda
wa polisi mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow.
Kati ya watu hao watano wametiwa mbaroni Mwanza na watu watano kutoka Dar es Salaam.
Leo
mjini Mwanza, mbele ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania IGP Said
Mwema, Mkurugenzi wa makosa ya Jinai Nchini (DCI) Robert Manumba
aliwataja watuhumiwa hao ni Muganizi Michael Peter (36) mkazi wa
Isamilo ambaye inadaiwa alikiri mwenyewe kumuua kamanda kwa risasi.
Wengine
ni Chacha Waitara Mwita (50), Magige Mwita Marwa, Bugazi Edward Kusota
na Bhoke Mara Mwita (42) ambao walikamatwa jijini Dar es Salaam baada ya
kuwekewa mtego kwa msaada wa wananchi.
Wanaoshikiliwa
jijini Mwanza kwa mahojiano ni pamoja na Mwalimu Doroth Moses Lyimo
aliyekuwa na RPC wakati mauaji yakitokea, Felix Felician Minde (50),
Philemon Felician (46) maarufu kama Fumo, Bahati Agustino Lazaro (28) na Amos Magoto (30) maarufu kama Bonge.
Manumba
amesema simu iliyoporwa ya mwanamama ambaye alikuwa akisindikizwa
nyumbani na marehemu, ndiyo imesaidia kukamilisha upelelezi huo na
hatimaye wahusika kukamatwa.
Alisema Kikosi kazi cha upelelezi
kilichokuwa chini yake Manumba kilijigawa kwenye makundi matatu moja
ni lile la Ukamataji, Mahojiano na lingine la interejensia huku
wakitumia njia ya sanyansi kwa kufuatia mitandao ya simu.
Marehemu
Kamanda Barlow aliuawa usiku wa Oktoba 12 majira ya kati ya saa 7 na 8
usiku katika eneo la Mianzi Mitatu, Kitangiri, kona ya Bwiru baada ya
kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wakati
alipopita kumsindikiza Mwalimu Dorothy Moses nyumbani kwake kutoka
katika kikao cha harusi kilichofanyika Mtaa wa Rufiji.
---
Taarifa via blogu za GSengo na Lukwangule Ent.