WADAU wa usafiri wa Reli nchini wamepinga mapendekezo ya Shirika la
Reli Tanzania (TRL) na Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) la
kutaka nauli ya usafiri wa umma wa treni jijini Dar es Salaam kuwa Sh
700 na 800.
Aidha
wamesema ili kupunguza gharama za uendeshaji wameiomba serikali kutoa
ruzuku ili kusaidia kufikia lengo la kuleta usafiri huo kupunguza
msongamano na shida ya usafiri, kwani kwa gharama hizo watashindwa
katika ushindani wa daladala kutokana na wananchi kushindwa kulipa
nauli.
Wadau hao
wametoa maoni hayo leo wakati wa mkutano wa kukusanya maoni kuhusu
mapendekezo ya nauli za usafiri huo kutoka kwa TRL na TAZARA,
ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA).
Katibu
Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma ya Usafiri wa Nchi
Kavu na Majini (SUMATRA CCC), Oscar Kikoyo akitoa maoni ya baraza
alisema usafiri wa treni ya abiria hutolewa kama huduma sio biashara na
huendeshwa kwa ruzuku ya fedha ya walipakodi au biashara nyingine.
Alisema nauli ya Sh 800 ni kubwa ikilinganishwa na daladala na sio
sahihi kwa wote hata wanaoshuka kituo cha pili kulipa nauli sawa.
Alisema usafiri huo unaingia kwenye ushindani na daladala ili kupata
abiria hivyo kwa bei hiyo watumiaji watabaki kwenye daladala na magari
binafsi.
Baraza
lilipendekeza Sh 350 kwa mtu mzima na Sh 150 kwa wanafunzi huku
serikali ikitoa ruzuku ya uendeshaji wa treni ya abiria kwa wenye
ulemavu na wazee pamoja na kuondoa ushuru kwenye mafuta yanayotumika kwa
treni za abiria na kupendekeza treni hiyo kufanya kazi kuanzia saa 11
alfajiri hadi 3 usiku kwa siku saba za wiki.
Chama cha kutetea Abiria (Chakua) kilipendekeza nauli kuwa Sh 200 au
350 kwa watu wazima na Sh 50 kwa wanafunzi huku wakitaka serikali kuweka
ruzuku katika usafiri huo ili isitumike kama biashara bali huduma.
Mwenyekiti wa Chakua, Hassan Mchanjama alisema treni ifanye kazi muda
wote huku wakihakikisha usalama wa abiria, ikiwa ni pamoja na kuondoa
nyumba zote zilizo pembeni mwa reli.
Mfanyakazi mstaafu wa Reli, Boaz Mollel alitaka katika usafiri huo
kushirikisha sekta binafsi huku wakiwekeza katika usafiri maalumu wa
reli za mijini na iliyopo sasa iwe ya kuanzia kwani licha ya kuwa na
tatizo kuwalipa watu fidia, itasaidia kuwa na usafiri wa kisasa.
Meneja Masoko Mfawidhi wa TRL, Hassan Shaban alisema kutakuwa na treni
mbili zitakazosafiri kati ya Stesheni na Ubungo kupitia Buguruni
Mnyamani na kufanya safari zake asubuhi kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa
4 asubuhi na kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 2 usiku.
Alisema wanatarajia treni hizo zitabeba abiria 900 kwa safari moja
huku kukiwa na safari 12 . Alitaka nauli ziwe Sh 800 kwa watu wazima na
Sh 100 kwa wanafunzi.
Alisema watatumia Sh milioni 5.7 kwa siku katika kutoa huduma. Meneja
usalama wa Tazara, Hanya Mbawala aliwasilisha mapendekezo yake kutaka
nauli iwe Sh 700 kwa watu wazima na wanafunzi Sh 100 na kufanya safari
kati ya Mwakanga-Kurasini kupitia Stesheni ya Dar es Salaam na watatoa
huduma siku za kazi pekee na kufanya safari 24.
Akifunga mkutano huo, aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano huo wa jana,
Linford Mboma alishauri ili kukabiliana na ushindani katika soko la
usafirishaji abiria, alitaka nauli ipungue na kuwa nusu ya mapendekezo.
Awali Kaimu Meneja wa SUMATRA, Ahamad Kilima alisema mapendekezo
yaliyowasilishwa jana yatatolewa uamuzi mapema kwani usafiri wa reli
jijini unatarajiwa kuanza rasmi kutumika wiki ijayo.
--
Habari imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko via HabariLeo