Tuesday, October 23, 2012

WATENGENEZA ARV WASEMA KAMWE HAWACHI KUZALISHA ARV


UONGOZI wa kiwanda cha kutengeneza dawa za kupunguza makali ya Ugonjwa wa UKIMWI (ARV) cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI), umesema hautasitisha uzalishaji wa dawa hizo kwa kuwa hauna barua inayowakataza kufanya hivyo kutoka mamlaka yoyote.

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku 12 baada ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi kutangaza kufungia uzalishaji wa dawa hizo katika kiwanda hicho.

Mkurugenzi Mkuu wa TPI, Ramadhani Madabida alisema jana kwamba kiwanda hicho bado kinaendelea kuzalisha dawa hizo kwa kuwa hakuna barua kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyowataka wasimamishe uzalishaji huo.

“Wenye mamlaka ya kukifungia kiwanda chochote cha dawa na kukithibitisha ni TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania), siyo Wizara ya afya,” alisema.

Alisema baada ya tukio hilo, TFDA iliwataka kwa barua, watoe maelezo ndani ya siku 14 kuhusu mzunguko wa dawa hizo na siyo kusitisha uzalishaji... “Sisi tuliletewa barua na TFDA ambayo ilitutaka tutoe maelezo ndani ya siku 14 kuhusu dawa feki za ARV zilizosambazwa na kudaiwa kuwa ni za kwetu na tuliwaeleza.”

Alisema walifanya hivyo kwa wakati na TFDA iliwahakikishia na kuwathibitishia kuwa hizo dawa hazikutengenezwa katika kiwanda hicho.

“Sisi hatuna uwezo wa uelewa wa utengenezaji wa dawa za ARV bandia zilizokutwa katika mzunguko, wenyewe wanajua zilipotengenezwa na si hapa, ni nje ya nchi na wanafahamu kinachoendelea,” alisema Madabida.

Alisema kiwanda hicho kinazalisha dawa hizo kama kawaida na hawana kitu cha kuwakwaza kutoendelea na uzalishaji.

Alisema wanatarajia kuongeza uzalishaji kwa asilimia 70 na Desemba mwaka huu wanatarajia kuzindua kiwanda kipya ambacho kitakuwa kikifanya kazi chini ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na kitakapokamilika, kitakuwa na uwezo wa kuuza dawa hizo ndani na nje ya Tanzania.

Pia alisema wanachukua hatua zao na kuhakikisha umma  unaelezwa ukweli wa dawa za ARV bandia zilipopatikana.

Hata hivyo, kauli ya Madabida ilipingwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Donald Mmbando aliyesema jana kuwa kiwanda hicho kilipelekewa barua ya kujieleza na kusitisha uzalishaji ndani ya siku 14.

“Tuliletewa nakala ya barua kutoka TFDA ambayo wamemwandikia mmiliki wa kiwanda cha TPI kuwa atoe maelezo ndani ya siku 14 na kusitisha uzalishaji wa dawa hizo… Mmiliki anavyodai hajapewa barua, si kweli,” alisema Dk Mmbando.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFDA, Dk Hiiti Silo na Ofisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Gaudensia Simwanza hawakupatikana jana kutoa ufafanuzi juu ya sakata hilo baada ya simu zao kutopatikana.