Monday, October 22, 2012

TV ZENYE MIGONGO ZITAPOKEA MATANGAZO YA DIGITAL


Na Mohammed Mhina, Zanzibar

Imeelezwa kuwa TV zote zikiwemo zile zenye migongo, matumbo na viuno virefu zote zina uwezo sawa wa kupokea matangano ya digitali na Watanzania waepuke uvumi wa watu wachache wanaodai kuwa TV za zamani hazitapokea zitafutwa mara Tanzania itakapoingia kwenye mfumo wa Digitali.

Wito huo umetolewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano hapa nchini TCRA ambaye pia na Mratibu wa Ofisi za Kanda Bw. Victor Nkya, wakati wa mkutano wa Wataalamu wa Mawasiliano ya Habadi kwa njia ya digitali kutoka nchi za SADC unaojadili umuhimu wa mfumo wa Digitali.

Bw. Nkya amesema kuwa wananchi hawana haja ya kuwa na hofu juu ya TV walizonazo zikiwemo zenye matumdo na migongo mikubwa kuwa hazitaweza kupokea matangazo ya televishen katika mfumo mpya wa digitali.

Amesema kutokana na watu wengi kutumia televishen za Analojia, ni lazima kila mmoja wetu awe na kingamuzi na kazi ya Mamlaka ya mawasiliano ni kuwajengea wananchi matumaini na kuepuka kudanganywa.

Kwa siku za hivi karibuni baada ya Tanzania kuridhia mabadiliko ya mfumo wa Digitali, wananchi wamekubwa na wasiwasi wakidhani kuwa huo ndio mwisho wa tv za zamani.

Awali akifungua Mkutano huo wa siku tatu hapa mjini Zanzibar, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Rashid Suleiman, amewataka wananchi kukabiliana na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza wakati wa mabadiliko ya kutoka katika mfumo wa analojia na kuingia katika digitali.

Amesema ni vema wananchi wakahama mapema kutoka katika mfumo huo wa zamani ili kuepuka usumbufu wakati yatakapotokea mabadiliko hayo kwani hakutakuwa na muda wa nyongeza kama Watanzania walivyozoea.