Tuesday, October 23, 2012

MAHAKAMA KUU ARUSHA YAMWACHIA HURU MGONJA

Habari hii imeandikwa na Woinde Shizza via blog
MAHAKAMA  kuu  kanda ya  Arusha, imemwachia huru aliyekuwa Katibu wa Mbunge wa Arusha mjini Gervas Mgonja pamoja na watuhumiwa wengine wawili, baada ya mahakama hiyo kuthibitisha  kutokuwa na kesi ya kujibu iliyokuwa ikiwakabili  mahakamani  hapo.

Akitoa maamuzi madogo (rulling)  mahakamani hapo, Hakimu Mkazi  wa mahakama kuu, Judith Kamala kwa kushirikiana na Mwendesha mashtaka wa Serikali, Haruna Matagane alisema kuwa, mahakama imeamua kumwachia huru mshitakiwa huyo na wenzake wawili baada  ya kubaini kuwa hawana kesi ya kujibu katika shitaka la kula njama na kutenda kosa lililokuwa likiwakabili.

Mgonja  alishtakiwa na wenzake wawili - aliyekuwa katibu wa vijana wa CHADEMA wilaya ya Arusha, Arnold Kamnde na Frank Njau aliyekuwa Katibu wa Vijana kata ya Ngarenaro CHADEMA.

Baada ya kupitia upande wa ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ambao walileta mashaidi sita, Hakimu Kamala alisema washtakiwa hao watatu kwa pamoja walikuwa wakishitakiwa na wenzao wengine watatu (jumla sita) kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha ambapo upelelezi ulipokamilika ulibaini kuwa washitakiwa watatu akiwemo Mgonja  walifungliwa shitaka hilo la unyang’anyi wa kutumia silaha kimakosa na hivyo mahakama kuwaondoa katika shitaka hilo na kubakia na washatakiwa watatu ambao wanaendelea na kesi hiyo.

Washitakiwa waliobakia na kesi hiyo ni Frank Ismail, Philemon Inyasi na Charles George.

Awali, Mgoja na wenzake walikaa ndani kwa siku 120 tangu walipofunguliwa shitaka hilo Agosti 20 mwaka jana hadi upelelezi ulipokamilika Januari 15 mwaka huu na  kuwaondoa katika kesi hiyo na kusomewa shitaka jipya la  kula njama ya kutenda kosa, ndipo walipopewa dhamana.

Kesi hiyo mpya  ilianza kusikilizwa  Januari 15 mwaka huu na  kesi  ilirindima kwa kipindi cha miezi kumi hadi maamuzi madogo ya mahakama  yalipotolewa kuwa washitakiwa hawana shitaka la kujibu.

‘Kutokana na kusikiliza upande wa mashahidi kwa makini,  nimetosheka na ushahidi uliotolewa na mahakama  na nimemwachia huru  Gervas Mgonja na wenzake wawili  na kuwa hawana kesi ya kujibu,’ alisema Kamala.

Akizungumza mara baada ya maamuzi hayo, Gervas Mgonja alisemaanamshukuru Mungu sana kwani haki imeweza kutendeka na leo hii ameachiwa huru pamoja na kuwa kesi zote hizo alibambikiziwa, ‘Kwa kweli sijui hata niseme nini... namshukuru Mungu  kwa  kunitetea na kesi yangu imeisha na leo hii nipo huru. Kwa kweli sina cha kusema ila  nawaomba polisi  wawe  makini kabla ya kuchukua hatua,  wafanye uchunguzi  ili waweze kuwatendea haki sawa raia wote.’

Alitoa wito kwa  jeshi la polisi kuwa makini katika utendaji wake ili kuepuka uonevu mkubwa unaofanyika kwa kuwafungulia watu kesi ambazo hawakuhusika kitendo kilichosababisha kukaa ndani miezi 5 na baadaye kuogundulika kuwa alifunguliwa shitaka hilo kimakosa kutokana na jeshi hilo kutokuwa makini.